Mar 29, 2024 11:58 UTC
  • Watu 38 wauawa katika hujuma za anga za Israel Syria, Iran yalaani

Kwa akali watu 38 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mji wa Aleppo (Halab) huko kaskazini mwa Syria.

Shirika la habari la Iran Press limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, jeshi la utawala wa Kizayuni limefanya mashambulizi hayo ya kichokozi kwa kutumia ndege zisizo na rubani (droni).

Shirika la Syrian Observatory for Human Rights lenye makao yake nchini Uingereza limedai kuwa hujuma hizo za anga za Israel zimelenga hifadhi ya silaha karibu na Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Aleppo na kusababisha miripuko kadhaa.

Habari zaidi zinasema kuwa, utawala wa Kizayuni umeshirikiana na makundi ya wabeba silaha ambayo hayakutajwa majina kutekeleza chokochoko hizo mpya zilizopelekea kuuawa makumi ya wanajeshi na raia wasio na hatia wa Syria.

Mji wa Aleppo ulivyoharibiwa na mashambulizi ya maadui

Mwakilishi wa Kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa mara kwa mara amekuwa akilaani wimbi la mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mji wa Aleppo (Halab) huko kaskazini mwa Syria na kusisitiza kuwa, uvamizi huo unakanyaga sheria za kimataifa, Hati ya Umoja wa Mataifa mbali na kuwa tishio kubwa kwa amani na uthabiti wa eneo la Asia Magharibi.

Kabla ya Aleppo kukabiliwa na mradi wa uasi ulioanza kutekelezwa na maadui wa Syria mwaka 2011, ulihesabiwa kuwa mji mkuu wa kiuchumi wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Wakati huo huo, Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali mashambulizi hayo ya anga ya Israel nchini Syria, na kuyataja kuwa ni kosa la kimkakati na ukiukaji wa mamlaka na mipaka ya nchi hiyo, sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.

Tags