Afrika ingali na uwezo wa kuvutia uwekezaji
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i14089-afrika_ingali_na_uwezo_wa_kuvutia_uwekezaji
Waziri Mkuu wa Japan ameanza ziara yake ya siku mbili huko Kenya kwa lengo la kushiriki katika Kongamano la Kimataifa la Tokyo kwa ajili ya Ustawi wa Afrika mashuhuri kama TICAD.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 27, 2016 23:32 UTC
  • Afrika ingali na uwezo wa kuvutia uwekezaji

Waziri Mkuu wa Japan ameanza ziara yake ya siku mbili huko Kenya kwa lengo la kushiriki katika Kongamano la Kimataifa la Tokyo kwa ajili ya Ustawi wa Afrika mashuhuri kama TICAD.

Katika safari hiyo, Shinzo Abe ameandamana  na wakuu na wakurugenzi wa mashirika makubwa ya kiuchumi ya Japan zaidi ya 80. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa Japan wapo Nairobi kwa minajili ya kuimarisha uhusiano wa kifedha na kiuchumi na nchi za Kiafrika.

Rais Kenyatta akimkaribisha mgeni wake Shinzo Abe Waziri Mkuu wa Japan mjini Nairobi, 26 August 2016

Uimarishaji uwekezaji katika nchi mbalimbali za Kiafrika na kuzidisha ushirikiano baina ya maafisa wa kiuchumi wa Afrika na Japan ni miongoni mwa masuala  yatakayochunguzwa katika kongamano hilo. Aidha suala la uwekezaji katika sekta ya miundombinu ya nchi za bara la Afrika litajadiliwa katika kongamano hilo la kimataifa la TICAD. Kiwango cha ubadilishanaji wa kiuchumi kati ya Japan na Afrika kinafikia dola bilioni 25.

Weledi wa mambo wanasema kuwa si Japan pekee bali nchi nyingi  zenye uchumi uliostawi duniani kwa muda sasa zimekuwa zikiandaa misingi na mazingira ya lazima kwa ajili ya kuwekeza katika nchi za bara la Afrika.

Shinzo Abe akizungumza kwenye kikao cha utangulizi TICAD Nairobi, 26 Agust, 2016

Kuwa na uwezo na suhula bora za kiuchumi, madini muhimu, nguvukazi kazi ya kizazi cha vijana na kuwa na nafasi nzuri ya kijiografia, ni miongoni mwa suhula zilizopo Afrika zinazovutia uwekezaji wa kigeni barani humo.

Hata kama nchi koloni zikiwemo Ufaransa, Uingereza, na katika miongo ya hivi karibuni Marekani, zimekuwa zikijaribu kwa nguvu kunufaika na maliasili tajiri za nchi za Kiafrika ili kujidhaminia maslahi na kuimarisha uwepo wao barani Afrika, lakini kuanza harakati za kupigania uhuru za nchi nyingi za bara hilo na kuendeshwa mapambano dhidi ya siasa za kikoloni, kumepelekea katika miongo ya hivi karibuni kubadilika mchakato wa kisiasa na hali ya kiuchumi na kijamii katika aghalabu ya nchi za bara hilo.

Rais XI Jinping wa Uchina akikaribishwa na mwenyeji wake Jakaya Kikwete, Rais wa zamani wa Tanzania Nov.6, 2014 akiwa katika safari ya kuimarisha uhusiano wa nchi yake na nchi za bara la Afrika

Kuasisiwa mifumo ya kisiasa ya kidemokrasia, kufunguliwa vituo vya elimu na maendeleo ya uchumi kumebadili hali ya mambo katika nchi za Kiafrika katika miongo ya hivi karibuni na kuzifanya nchi nyingi duniani khususan zile zenye uchumi unaoibukia kama China kutaka kuwekeza barani Afrika.

Kutiwa saini makumi ya hati za maelewano kati ya Afrika na mashirika kumi ya China katika sekta za viwanda na madini ni moja kati ya mifano ya uwekezaji wa nchi hiyo barani Afrika. Mbali na nchi hizo, nchi kama Ufaransa,  Uingereza na Marekani pia zimebadili siasa zao na kubainisha mfumo mpya ili kuendeleza ukoloni wao barani Afrika; na wakati huo huo kufanya juhudi za kuimarisha uwepo wao Afrika kwa anwani mbalimbali kama eti kusaidia kuleta demokrasia na kutoa mikopo ya muda mrefu na misaada mingine katika sekta za kiuchumi ili kufikia lengo hilo.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, mmoja wa viongozi wakongwe barani Afrika wasiotaka kuondoka madarakani

Katika upande mwingine viongozi wengi wa bara la Afrika hawako tayari kuondoka madarakani na kuheshimu kura za wananchi wao licha ya kuweko uongozini kwa miaka mingi.

Kujiri vita vya kikabila vinavyosababisha ukosefu wa amani na pia kukosekeana miundo mbinu ya ustawii kama barabara na mabwawa ya kuzalisha umeme, ni matatizo mengine yanayokwamisha uwekezaji barani Afrika.

Pamoja na hayo yote, wataalamu wengi wa masuala ya kiuchumi wanaamini kuwa sehemu kubwa ya uchumi wa dunia utakuwa ukidhibitiwa na nchi za Kiafrika katika miongo ijayo na kwamba nchi za bara hilo zitakuwa na nafasi muhimu katika biashara ya kimataifa. Kwa msingi huo, inaonekana kuwa mchuano mkali umeanza kati ya nchi mbalimbali kwa ajili ya kuwekeza barani Afrika. Kuwepo Waziri Mkuu wa Japan na ujumbe wa kiuchumi wa nchi yake anaoandamana nao huko Kenya pia kunapasa kutathminiwa katika uwanja huo.