Mpaka wa Iran na Pakistan kuwa eneo la amani na urafiki
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i38275-mpaka_wa_iran_na_pakistan_kuwa_eneo_la_amani_na_urafiki
Msemaji wa jeshi la Pakistan ametangaza kuwa, mpaka wa nchi hiyo na Iran utafanywa kuwa mpaka na eneo la amani na urafiki kwa maana halisi ya neno hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 30, 2017 00:56 UTC
  • Mpaka wa Iran na Pakistan kuwa eneo la amani na urafiki

Msemaji wa jeshi la Pakistan ametangaza kuwa, mpaka wa nchi hiyo na Iran utafanywa kuwa mpaka na eneo la amani na urafiki kwa maana halisi ya neno hilo.

Jenerali Asef Ghafur ameashiria juhudi zinazofanywa na pande hizo mbili kwa ajili ya kuufanya mpaka wa Iran na Pakistan kuwa eneo la amani na urafiki na kusema: Vituo vipya vya mpakani vinajengwa kwa ajili ya kurahisisha safari za raia wa pande mbili na wakazi wa maeneo ya mpakani.

Nchi mbili za Iran na Pakistan zina mpaka wenye urefu wa zaidi ya kilomika mia tisa na kwa miaka mingi eneo hilo limekuwa miongoni mwa mikapa yenye amani na usalama zaidi katika eneo hili la Asia. Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni na kutokana na kushadidi harakati za makundi ya kigaidi na makundi hayo kuwa wenzo na fimbo inayotumiwa na maadui wa mataifa mawili ya Waislamu wa Iran na Pakistan, kumeshuhudiwa baadhi ya harakati chafu za kigaidi katika mpaka wa nchi mbili. Uzembe wa serikali na jeshi la Pakistan katika kudhamini amani na usalama wa maeneo ya mpakani umewafanya baadhi ya watu waovu kukimbilia katika ardhi ya nchi hiyo baada ya kufanya uhalifu nchini Iran. Hali hiyo imetoa changamoto kubwa ya uhusiano wa Iran na Pakistan katika miaka ya hivi karibuni. Kwa kadiri kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetishia kuwa iwapo mashambulizi ya kigaidi yataendelea kuvuka mipaka ya Pakistan na kuilenga Iran, jeshi la mpakani la Jamhuri ya Kiislamu yumkini likawafuata wahalifu hao ndani ya ardhi ya Pakistan.

Magaidi wanaotumiwa kuvuruga amani na usalama mpaka wa Iran na Pakistan

Asef Izadi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya siasa wa Pakistan anasema: "Chokochoko zinazofanywa na baadhi na makundi ya wahalifu katika mpaka wa Iran na Pakistan ambazo zimepungua kwa kiwango kikubwa katika miaka ya hivi karibuni zinapaswa kudhibitiwa. Ushirikiano wa masuala ya usalama kati ya Iran na Pakistan pia unapaswa kuimarishwa zaidi na suala hilo linaweza kusaidia sana katika uwanja huo."

Kwa kutilia maanani ukweli huo, askari wa vikosi vya walinzi wa mipaka wa Iran na Pakistan wamekubaliana kuanzisha doria ya jeshi la anga kwa shabaha ya kulinda amani katika maeneo ya mpakani na kupambana na magaidi. Suala hilo lina umuhimu mara dufu kwa Pakistan hasa kwa kutilia maanani juhudi zinazofanywa na nchi hizo mbili kwa ajili ya kupanua zaidi ushirikiano wa kiuchumi na vilevile udharura wa kulinda amani na usalama wa eneo hili kwa ajili ya utekelezaji wa mipango kabambe ya kiuchumi.

Miradi mikubwa ya kiuchumi inafanyika kati ya Iran na Pakistan

Hassanain Reza Miirreza ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi wa Pakistan anasema: "Kambi ya kiuchumi inayoundika kwa sasa katika eneo hili la Asia ambayo inajumuisha nchi za Iran na Pakistan, inatarajiwa kuwa kituo muhimu cha kiuchumi kwa sharti la kudhaminiwa amani na usalama hususan katika jimbo la Baluchistan la Pakistan linalopakana na Iran."

Vilevile inatupasa kuelewa kwamba, kila mwaka maelfu ya wafanya ziara wa Pakistan husafiri kupitia mipaka ya nchi kavu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na suala hilo pia linakabiliwa na changamoto kubwa ya mashambulizi ya kigaidi. Kwa msingi huo kuna udharura wa jeshi la Pakistan kuchukua hatua za dharura na kushirikiana kikamilifu ya askari walinzi wa mipaka wa Iran kwa ajili ya kulinda amani na usalama wa maeneo hayo na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi, uwekezaji wa pande mbili na usalama wa safari za wafanya ziara na watalii wa nchi hizo mbili.