China yaikosoa Marekani kwa kuanzisha vita vya kibiashara duniani
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i46887-china_yaikosoa_marekani_kwa_kuanzisha_vita_vya_kibiashara_duniani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameikosoa Markeani kwa kuanzisha vita vya kibiashara duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 19, 2018 22:17 UTC
  • China yaikosoa Marekani kwa kuanzisha vita vya kibiashara duniani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameikosoa Markeani kwa kuanzisha vita vya kibiashara duniani.

Katika mkutano na waandishi habari mjini Beijing, Hua Chunying amesema vita vya kibiashara vilivyoanzishwa na Marekani si tu kuwa vitapelekea China ihasimiane na Marekani bali pia vitasababisha kuongezeka uhasama baina ya Washington na mataifa mengine mbali na kusababisha matatizo ya kiuchumi duniani.

Huku akiashiria kuwa Marekani imeanzisha vita hivyo vya kibiashara duniani kwa lengo la kukidhi maslahi yake binafsi, ameongeza kuwa vita vya kibiashara vilivyoanzishwa na Marekani vitapelekea kudororoa ustawi wa kibiashara duniani na kusababisha nchi mbali mbali zisiwe tena na imani na uchumi wa dunia.

Ingawa Marekani inadai kuwa, hatua yake ya kuongeza asilimia 25 ya ushuru unaotozwa bidhaa zinazoingizwa kutoka Marekani inalenga kuilazimu nchi hiyo kufidia ukosefu wa mlingano wa biashara kati yake na Marekani, lakini serikali ya Beijing inasema inasisitiza vita hivyo vya kibiashara si dhidi ya China tu bali ni dhidi ya dunia nzima.

Rais Donald Trump wa Marekani anadai kuwa, matatizo mengi ya kiuchumi nchini humo yanatokana na kuwa China imeweza kuingia kwa urahisi katika soko la Marekani.

Hii ni katika hali ambayo, Marekani haijaongeza tu ushuru wa bidhaa zinazongizwa kutoka China, bali pia imeanzisha vita vya kibiashara na waitifake wake hasa katika Umoja wa Ulaya. Weledi wa mambo wanasema mashirika ya Marekani yatapata hasara zaidi kutokana na vita hivyo vya kibiashara vilivyoanzishwa na Trump kwani yatapoteza hisa yao ya uzalishaji bidhaa nchini China ambayo ni kati ya masoko muhimu zaidi duniani.

Rais Trump wa Marekani

Scott Kennedy, mtaalamu wa masuala ya kiuchumi anasema: 

Hivi sasa kuna mashirika ya kimataifa yaliyoko nchini China na yanashindana katika  soko la dunia. Kwa hivyo mashirika hayo yana wasiwasi mkubwa kuhusu vita vya kibiashara baina ya Marekani na China kwani hali hiyo inaweza kuvuruga biashara ya dunia na kusababisha matatizo mengi.

Hata kama Trump anajaribu kuongeza ushuru wa forodha wa bidhaa zinaoziongizwa nchini humo kutoka nchi mbali mbali, ikiwemo China ili kwa njia hiyo kuboresha uchumi na sekta ya viwanda Marekani na kupunguza ukosefu wa ajira, lakini kwa kuzingatia kuwa uchumi wa Marekani umefungamana pakubwa na uchumi  wa dunia, vita vya kibiashara vilivyoanzisha na Trump vitaidhuru pia nchi hiyo.

Hii ina maana kuwa China na nchi zinginezo nazo pia zitachukua hatua mshabaha kwa lengo la kukabiliana na sera za Marekani za kulinda mashirika yake. Kati ya hatua hizo ni kupiga marufuku bidhaa zinazoingizwa kutoka Marekani na hilo linaweza kutoa pigo kubwa sana kwa tabala la kati la jamii ya Marekani.

Wang Shu Van, mtaalamu wa masuala ya kibiashara nchini China anasema: 

"Sera za Marekani zitatoa pigo kwa maslahi ya China na kuhatarisha usalama wa kiuchumi wa nchi hiyo. Aidha Marekani inahatarisha uthabiti wa uchumi wa dunia. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kipengee cha saba cha sheria za biashara za kigeni  nchini China, nchi yoyote  itakayochukua hatua za kibaguzi dhidi ya China kama vile kupiga marufuku au kuweka vizingiti itakabiliwa na hatua mshabaha. Kwa hivyo China italazimika kuchukua hatua mkabala kukabiliana na Marekani."

Mabadilishano ya kibiashara yataathiriwa vibaya na vita vya kiuchumi vilivyoanzishwa na Trump

Kwa vyovyote vile, hakuna shaka kuwa, vurumai zilizoibuliwa na Rais Trump wa Marekani katika uga wa biashara ya kimataifa na soko la mafuta duniani ni mambo yatakayotoa piga kwa uchumi wa dunia.

Ni kwa sababu hii ndio pamoja na kuwepo jitihada za Marekani, hata waitifaki wa nchi hiyo hawako tayari kutwishwa mzigo wa sera ghalati  za kiuchumi za Ikulu ya White House dhidi ya nchi zingine za dunia.