Ripoti: Israel imeua Wapalestina 200 na kukamata watoto 570, 2023
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i100252-ripoti_israel_imeua_wapalestina_200_na_kukamata_watoto_570_2023
Vikosi vya usalama vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimewaua shahidi mamia ya Wapalestina kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu 2023 hadi sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 24, 2023 07:31 UTC
  • Ripoti: Israel imeua Wapalestina 200 na kukamata watoto 570, 2023

Vikosi vya usalama vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimewaua shahidi mamia ya Wapalestina kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu 2023 hadi sasa.

Ripoti mpya imeeleza kuwa, utawala huo haramu umewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 200 tokea Januari mwaka huu hadi sasa katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kanali ya Press TV imenukuu ripoti hiyo ikieleza kuwa, utawala huo pandikizi unawaua shahidi Wapalestina wakiwemo watoto wadogo na wanawake kila uchao mkabala wa kimya cha jamii ya kumataifa.

Aidha ripoti mpya iliyotolewa na kituo cha kutetea maslahi ya wafungwa wa Palestina cha PCPS imesema maafisa usalama wa utawala wa Kizayuni wamewatia mbaroni mamia ya watoto wa Kipalestina tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Riyad al-Ashqar amesema watoto wasiopungua 570 wa Kipalestina wametekwa nyara na vyombo vya dola vya Wazayuni tokea Januari mwaka huu mpaka sasa.

Amesema kumenakiliwa ongezeko la asilimia 15 ya kamatakamata hiyo ya watoto wa Kipalestina hususan katika mji mtukufu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu mwaka huu, ikilinganishwa na mwaka jana. 

Al-Ashqar ameeleza kuwa, miongoni mwa mamia ya watoto wa Kipalestina waliokamatwa na kutekwa nyara na Wazayuni mwaka huu, 29 wana umri wa chini ya miaka 12, na wengine wawili wana miaka 10 pekee. 

Takwimu za Klabu ya Wafungwa wa Kipalestina (PPC) zinaonesha kuwa, kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, Wapalestina zaidi ya 3000 wamekamatwa na askari makatili wa Kizayuni. Mwaka jana, Wapalestina zaidi ya 7000 wakiwemo wanawake na watoto wadogo walitiwa mbaroni na vyombo vya usalama vya utawala pandikizi wa Israel.