Jenerali wa Israel akiri; Nasrullah si mtu wa kupuuzwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i100580-jenerali_wa_israel_akiri_nasrullah_si_mtu_wa_kupuuzwa
Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Operesheni cha jeshi la utawala haramu wa Israel amesema Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ni shakhsia ambaye hapaswi kupuuzwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 01, 2023 22:49 UTC
  • Jenerali wa Israel akiri; Nasrullah si mtu wa kupuuzwa

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Operesheni cha jeshi la utawala haramu wa Israel amesema Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ni shakhsia ambaye hapaswi kupuuzwa.

Meja Jenerali mstaafu Israel Ziv amesema hayo katika mahojiano na kanali ya 12 ya televisheni ya Kizayuni na kuongeza kuwa, Nasrullah ni mweledi na mahiri, na kwa msingi huo haifai kumpuuza hata kidogo.

Jenerali huyo wa Kizayuni ameungama na kusema, "Nasrullah anafahamu vizuri matukio yanayofanyika katika ardhi zinazokaiwa kwa mabavu, na hili linathibitishwa na nadharia yake ya kuifananisha Israel na nyumba ya buibui ambayo aliitoa baada ya ukombozi wa eneo la kusini mwa Lebanon mwaka 2000."

Afisa huyo wa zamani wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel ameendelea kufafanua zaidi kwa kusema: (Nasrullah) anasoma magazeti yetu kila asubuhi, anafuatilia habari zetu, na pengine anatutazama tunapozungumza kwenye televisheni; na kupitia darubini hiyo, anaelewa na anaona Israel inavyoporomoka na kuparaganyika.

Jenerali Ziv amesema kuwa, Nasrullah ana uelewa mpana wa matukio ya eneo, na ndiyo maana daima analidogosha baraza la mawaziri la Netanyahu, na kuudhalilisha utawala wa Kizayuni kwa kuanika mapungufu yao. 

Matamshi ya jenerali huyo wa kijeshi wa Israel yametolewa siku chache baada ya Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kusema kwamba, Israel licha ya kumiliki silaha za nyuklia na kuwa na nguvu kubwa ya kijeshi katika eneo hili, lakini ni dhaifu sana kuliko nyumba ya buibui.