Hizbullah: Saudia inazuia kufanyika uchaguzi wa rais Lebanon
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameikosoa vikali Saudi Arabia kwa kukwamisha mikakati ya kisiasa sambamba na kuzuia juhudi za kufanyika uchaguzi wa rais nchini Lebanon.
Sheikh Naeem Qassim amesema ombwe la uongozi linaloshuhudiwa hivi sasa nchini Lebanon limesababishwa na vizingiti vya utawala wa Riyadh na waitifaki wake nchini humo. Sheikh Qassim amesema Saudia imekuwa ikikataa kuheshimu mapendekezo mbali mbali yanayotolewa kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo wa kisiasa nchini Lebanon na hususan mapendekezo yanayoendana na matakwa ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu. Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, harakati hiyo ya muqawama tayari imeanzisha ramani ya njia ambayo iwapo Saudia na vibaraka wao nchini Lebanon wataiafiki, yumkini uchaguzi wa rais ukafanyika hata kesho. Kipindi cha urais wa Michel Sulaiman kilimalizika mwezi Mei 2014, lakini hadi hivi sasa hakuna rais mpya aliyechaguliwa. Alkhamisi iliyopita, Bunge la Lebanon kwa mara nyingine tena lilishindwa kumchagua rais mpya wa nchi hiyo kwa mara ya 41, kutokana na ukosefu wa akidi katika kikao hicho. Spika wa Bunge hilo Nabih Berri ametangaza tarehe 13 Julai kuwa siku ya kufanyika kikao kipya cha kumchagua rais wa Lebanon.