Askari makatili wa Israel wawaua shahidi vijana 2 wa Kipalestina Tulkarm
Wanajeshi vamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewaua shahidi vijana wawili wa Kipalestina katika mji Tulkarm, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Maafisa wa Wizara ya Afya ya Palestina wamesema vijana hao waliouawa shahidi jana Alkhamisi katika shambulizi la askari makatili wa Israel katika mji wa Tulkarm ulioko kaskazini magharibi ya Ukingo wa Magharibi ni Hudhayfah Fares na Abd al-Rahman Atta.
Shirika la habari la Wafa limenukuu maafisa wa Wizara ya Afya ya Palestina wakithibitisha habari ya kuuawa shahidi vijana hao wa Kipalestina kwa kupigwa risasi na Wazayuni. Fares alikuwa na umri wa miaka 23 na Atta 27.
Habari zaidi zinasema kuwa, vijana hao wanatoka katika kambi ya wakimbizi ya Tulkarm, na walikuwa wakiishi katika mji wa mashariki wa Dhanaba, katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu.
Haya yanajiri siku chache baada ya wanajeshi hao wa Kizayuni kuwaua shahidi Wapalestina wanne katika mashambulizi mawili tofauti katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.
Wapalestina zaidi 200 wameuawa shahidi na wanajeshi makatili wa Kizayuni tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, hasa katika eneo la Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.
Wimbi hilo la ukatili wa wanajeshi wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi linajiri wakati huu ambapo Wapalestina wameendelea kuandamana katika mpaka wa Gaza kulaani jinai za Wazayuni, kuendelea kuzuiliwa Wapalestina kinyume cha sheria, na kuvunjiwa heshima Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa.