Qatar yasikitishwa na utendaji kazi wa Baraza la Usalama huko Ghaza
Mwakilishi wa Qatar katika Umoja wa Mataifa amelalamikia siasa za utolewaji misaada ya kibinadamu huko Ghaza na kushindwa Baraza la Usalama kupitisha azimio kuhusiana na matukio ya eneo hilo.
Siku 19 zimepita tangu kuanza vita vya kikatili vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Wizara ya Afya ya Palestina katika ukanda huo imetangaza katika taarifa kwamba, idadi ya mashahidi wa eneo hilo tokea kuanza operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa Oktoba 7, imefikia watu 6,055 na majeruhi 15,143.
Nukta nyingine ni kwamba Kutokana na kuendelea kushambuliwa kwa mabomu maeneo ya makazi ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni, kwa ujumla aghalabu ya mashahidi na wahanga wa mashambulizi hayo ni wanawake, watoto na raia wa kawaida.
Gaza inashuhudia jinai za kivita na mauaji ya halaiki; makosa mawili ya jinai ambayo Jamii ya Kimataifa ina jukumu la kukabiliana na wahusika wake na hata inaweza kufuta kinga ya kushtakiwa wahalifu. Hata hivyo, siasa za madola makubwa kuhusiana na jambo hilo zinaonyesha kuwa vita vya Ghaza ni tukio la kisiasa zaidi kuliko la kijeshi.
Madola ya Magharibi ambayo yanadai kutetea haki za binadamu huku yakifumbia macho jinai za Wazayuni za kuua raia hususan watoto na wanawake wa Ghaza, sasa yanadai kuwa wakati wa kusitishwa vita huko Gaza bado haujafika.
Mratibu wa Mawasiliano ya Kistartijia ya Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani John Kirby ameashiria mashambulizi ya kijinai ya Israel kwenye Ukanda wa Ghaza na kusema kuwa Tel Aviv ina haki ya kujilinda kwa kuwalenga viongozi wa Hamas. Kirby amesisitiza kuwa hadhani ni sawa kusimamisha vita huko Ghaza.
Mtazamo huo wa serikali ya Marekani na nchi za Ulaya unaonyesha wazi kwamba wanachukulia vita vya Ghaza kuwa suala la kisiasa na kwa kuunga mkono mauaji ya raia wasio na hatia yanayofanywa na utawala wa Kizayuni, wanajaribu kufunika kushindwa Tel Aviv katika operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na hata kuzuia kutumiwa misaada ya kibinadamu huko Ghaza ili kufikia lengo lao hilo ovu.
Kwa msingi huo, katika kikao cha Jumatano usiku cha Baraza la Usalama, mwakilishi wa Qatar katika Umoja wa Mataifa alisema kuwa Doha ina hamu kubwa ya kupeleka misaada ya dharura katika Ukanda wa Ghaza, na kuongeza kuwa inapinga vikali kutumiwa kisiasa suala la kufikishwa misaada ya kibinadamu huko Ghaza.
Pia ameongeza kuwa Qatar inasikitika kuona kwamba Baraza la Usalama halikuweza kupitisha azimio kuhusu mapigano ya Ghaza, na kuwa amani inaweza kupatikana hata kwenye hali ngumu na hatari zaidi. Msimamo huo wa madola ya Magharibi kuhusu jinai za Wazayuni dhidi ya Ghaza unachukuliwa katika hali ambayo hata Antonio Guterres mwenyewe, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameeleza kuwa, mashambulizi ya Hamas katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hayakutokea kwenye ombwe na kuwa, wananchi wa Palestina wamekuwa chini ya mzingiro mkali kwa miaka 56. Amesema hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha mauaji na utekaji nyara wa raia au kurushwa makombora katika maeneo ya makazi ya raia
Hata hivyo Wazayuni na waungaji mkono wao, yaani Marekani na nchi za Ulaya pamoja na kumkosoa Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa bado wanaendelea kupinga kufikishiwa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Ghaza na kuunga mkono mashambulio ya kinyama yanayoendelea kufanywa dhidi yao.