Wapalestina 100 wameuawa shahidi katika hujuma mpya ya Israel huko Ghaza
Sambamba na kuanza operesheni ndogo ya nchi kavu ya jeshi katili la utawala haramu Israel kwa lengo la kujipenyeza Ghaza usiku wa kuamkia leo, zaidi ya raia 100 Wapalestina wameuawa shahidi huku utawala huo ukilaaniwa kote duniani kwa kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa ripoti ya Televisheni ya Al-Mayadeen siku ya Jumamosi, idadi ya mashahidi wa Kipalestina imeongezeka tangu kuanza kwa mashambulizi ya anga ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza. Utawala haramu wa Israel umevuruga na kuzima intaneti ya Ghaza ili kujaribu kuzuia habari za jinai zake kuwafikia walimwengu.
Duru za Palestina zimedokeza kuwa, tangu utawala katili wa Israel uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza, zaidi ya Wapalestina 7,400 wameuawa shahidi wakati wa mashambulizi hayo na wengine 18,000 wamejeruhiwa.
Aidha vyombo vya habari vya Palestina vimesema, katika shambulio la anga la jeshi katili la Israel dhidi ya jengo la makazi la Hayi al-Shati magharibi mwa Mji wa Ghaza, ambalo lilikuwa makazi ya wakimbizi, zaidi ya Wapalestina wapatao 100 wameuawa shahidi.
Jana usiku, vikosi vya Israel vilijaribu kuingia katika mipaka ya mashariki ya Ukanda wa Ghaza ambapo vilikumbana na wapiganaji shupavu wa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina. Makomando wa wa utawala wa Kizayuni wa Israel walifeli katika jitihada zao za kujipenyeza ndani ya Ghaza.
Ripoti zaidi zinaonyesha kuwa utawala haramu wa Israel ulitumia mabomu meupe ya fosforasi kaktika mashambulio yake ya jana dhidi ya Wapalestina. Utumizi wa mabomu ya fosforasi karibu na maeneo yenye raia wengi au dhidi ya raia ni jinai ya kivita kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Wizara ya Afya ya Palestina ilitangaza kuwa mashahidi wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wameongezeka hadi kufikia 110 na wengine zaidi ya 1,900 kujeruhiwa tangu Oktoba 7.
Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina katika Ukanda wa Gaza pia limeonya kwa kusema: Kwa sasa tunakabiliwa na janga la kiafya katika eneo hili kwa sababu Wapalestina wanalazimika kutumia maji ya kunywa yasiyo safi kiafya.
Msemaji wa Jumuiya ya Kulinda Wananchi wa Ghaza pia ametangaza kuwa, idadi ya Wapalestina walioachwa chini ya vifusi vya mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni ni zaidi ya 1,600.
Inafaa kuashiria hapa kuwa katika kukabiliana na jinai za Wazayuni, vikosi vya muqawama au wapigania ukombozi wa Palestina vilianzisha operesheni ya "Kimbunga cha Al Aqsa" huko Ukanda wa Ghaza dhidi ya ngome za utawala wa Kizayuni wa Israel kuanzia Jumamosi, Oktoba 7, 2023.
Tangu kuanza kwa operesheni hiyo, jeshi la Kizayuni, ambalo halina uwezo wa kukabiliana na wapiganaji wa muqawama, limekuwa likishambulia kwa mabomu maeneo ya raia, hospitali, vituo vya kidini na shule huko Ghaza.