Kituo cha jeshi la Marekani Iraq chashambuliwa, droni yake ya MQ-9 yatunguliwa Yemen
(last modified Thu, 09 Nov 2023 07:12:14 GMT )
Nov 09, 2023 07:12 UTC
  • Kituo cha jeshi la Marekani Iraq chashambuliwa, droni yake ya MQ-9 yatunguliwa Yemen

Vikosi vya Muqawama wa Kiislamu nchini Iraq vimeishambulia kambi ya jeshi la anga inayohifadhi wanajeshi wa Marekani nchini humo. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq imesema, jana ilikishambulia kituo cha jeshi la anga cha al-Harir kinachotumiwa na askari wa jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani kaskazini mwa nchi hiyo kwa kutumia ndege mbili zisizo na rubani.

Harakati hiyo imeeleza bayana kuwa hatua hiyo ni jibu kwa Marekani kutokana na uungaji mkono inaotoa kwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika mashambulio na mauaji ya kinyama unayoendelea kufanya dhidi ya watu wa Gaza.

Mashuhuda kadhaa wamesema, jana jioni, ving'ora vilisikika katika ubalozi wa Marekani katika eneo lenye ulinzi mkali la Ukanda wa Kijani mjini Baghdad ulipo ubalozi huo.

Wakati huo huo, vikosi vya jeshi la Yemen vimetangaza kuwa vimeiangusha ndege isiyo na rubani ya MQ-9 Reaper kwa kutumia kombora la ardhini kuelekea angani iliyokuwa ikiranda kwenye eneo la mpaka wa majini wa nchi hiyo.

Droni ya kisasa ya MQ-9 Reaper

Taarifa iliyotolewa na vikosi hivyo imesema droni hiyo ya kisasa ya Marekani ilikuwa ikifanya ikifanya operesheni ya kiuadui katika anga ya Yemen katika muendelezo wa usaidizi wa kijeshi wa Washington kwa utawala dhalimu wa Israel.

Hisia za chuki dhidi ya Israel na Marekani zinazidi kuongezeka katika eneo la Asia Magharibi kutokana na uungaji mkono wa kila hali inaotoa Washington kwa mashambulio ya kinyama na mauaji ya kikatili yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza uliowekewa mzingiro, ambayo hadi sasa yameshasababisha vifo vya watu wasiopungua 10,569, wakiwemo watoto 4,324.

Watu wengine 26,475 wamejeruhiwa, mbali na 2,550 ambao wameripotiwa kupotea, wakiwemo watoto ambao huenda wamekufa au wamenasa chini ya vifusi wakisubiri kuokolewa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, asilimia 70 ya wakazi wa Gaza wamebaki bila makazi baada ya kulazimika kuyahama makazi yao yaliyobomolewa kwa mabomu na makombora ya jeshi la utawala haramu wa Israel.../

Tags