Ripoti: Israel imeua makumi ya wanariadha wa Palestina tangu Oktoba 7
(last modified Sun, 10 Dec 2023 02:55:12 GMT )
Dec 10, 2023 02:55 UTC
  • Ripoti: Israel imeua makumi ya wanariadha wa Palestina tangu Oktoba 7

Israel imeua shahidi makumi ya wanariadha na wamamichezo wa Palestina tangu utawala huo wa Kizayuni uanzishe mashambulizi ya kutisha dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7.

Shirika rasmi la habari la Palestina la WAFA limenukuu ripoti ya Kamati ya Olimpiki ya Palestina iliyosema kuwa, “mashine ya maangamizi ya Israel” imeua wanariadha wasiopungua 47 wa timu na michezo mbalimbali wa Kipalestina tangu ilipoanzisha vita.

Aidha kamati hiyo imesema maafisa 17 watendaji na wa mabenchi ya ufundi ya michezo mbalimbali wameuawa pia katika hujumua hizo za Wazayuni dhidi ya Gaza ndani ya miezi miwili.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, miongoni mwa wanamichezo wa Kipalestina waliouawa shahidi katika hujuma hizo za utawala haramu ni Yasmine Sharaf, mwanakarate aliyekuwa na miaka sita na aliyekuwa na azma ya kuiwakilisha Palestina katika majukwaa ya kimataifa ya michezo.

Taarifa ya Kamati ya Olimpiki ya Palestina imeeleza kuwa, vikosi vya Israel vimeshambulia kwa mabomu na kuharibu viwanja na taasisi kadhaa za michezo za Palestina, ukiwemo Uwanja wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa UNDP, Uwanja wa Beit Hanoon pamoja na viwanja na kumbi nyingine za michezo huko Gaza.

Utawala huo katili umeua shahidi Wapalestina zaidi ya 17,000, aghalabu yao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo, tangu uanzishe mashambulizi ya kijinai dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7.