Jeshi la Yemen: Tumeshambulia kwa kombora meli iliyokuwa ikielekea Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i105924-jeshi_la_yemen_tumeshambulia_kwa_kombora_meli_iliyokuwa_ikielekea_israel
Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimekiri kuhusika na shambulizi la kombora la cruise dhidi ya meli ya mafuta katika Bahari Nyekundu, ikiwa njiani kuelekea katika bandari ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-12-12T23:16:00+00:00 )
Dec 12, 2023 23:16 UTC
  • Jeshi la Yemen: Tumeshambulia kwa kombora meli iliyokuwa ikielekea Israel

Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimekiri kuhusika na shambulizi la kombora la cruise dhidi ya meli ya mafuta katika Bahari Nyekundu, ikiwa njiani kuelekea katika bandari ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Msemaji wa jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree alisema hayo jana Jumanne mjini Sana'a na kuongeza kuwa, meli hiyo iliyoshambuliwa kwa kombora la cruise na vikosi vya Yemen ilikuwa na bendera ya Norway. 

Brigedia Jenerali Yahya Saree ameeleza kuwa: Shambulizi dhidi ya meli ya mafuta ya Strinda ni ushindi kwa Wapalestina wanaoendelea kuuawa shahidi kwa umati na utawala katili wa Israel huko Gaza.

Saree ameongeza kuwa, vikosi vya Yemen vilishambulia kwa usahihi mkubwa meli hiyo ya mafuta ikiwa karibu na Lango Bahari la Bab al-Mandab.

Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimetadharisha kuwa, vitazuia na kushambulia meli zote zinazoelekea Israel bila kujali ni za nchi gani.

Msemaji wa jeshi la Yemen amesisitiza kuwa, "Iwapo Ukanda wa Gaza hautapatiwa misaada ya chakula na dawa za matibabu; vikosi vyetu vya ulinzi vitazishambulia meli zote zilizoko katika Bahari Nyekundu kuelekea katika bandari za utawala wa Kizayuni wa Israel."

Tangu vita vya Gaza vianze Oktoba 7 mwaka huu, jeshi la Yemen limeanzisha operesheni mtawalia dhidi ya meli zenye mfungamano na utawala wa Kizayuni katika Bahari Nyekundu na kutekeleza mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni) dhidi ya ngome na maeneo mbalimbali ya Israel katika kuonyesha mshikamano na  wananchi wa Palestina waliozingirwa huko Gaza.