Kambi ya jeshi ya Ain al-Asad ya US huko Iraq yashambuliwa kwa droni
(last modified Fri, 15 Dec 2023 11:23:21 GMT )
Dec 15, 2023 11:23 UTC
  • Kambi ya jeshi ya Ain al-Asad ya US huko Iraq yashambuliwa kwa droni

Kwa mara nyingine tena, wanamuqawama wa Kiislamu wa Iraq wamewashambulia kwa ndege isiyo na rubani (droni) wanajeshi wa vikosi vamizi vya Marekani katika kambi ya Ain al Asad huko Iraq.

Hakuna taarifa iliyotolewa kufikia sasa kuhusu majeruhi wa shambulizi hilo la droni la usiku wa kuamkia leo katika mkoa wa Anbar, magharibi mwa Iraq.

Wanamuqawama wa Iraq wameshambulia kwa droni kambi hiyo ya anga ya vikosi vamizi vya Marekani huko Iraq, kama jibu kwa hatua ya Washington ya kuunga mkono kwa hali na mali hujuma za Israel dhidi ya Gaza, kufuatia Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa cha wanamuqawama wa Palestina.

Kwa mara kadhaa sasa kambi ya kijeshi ya anga ya vikosi vamizi vya Marekani huko al Anbar Iraq na vituo vingine vinavyodhibitiwa na jeshi la Marekani vimeshambuliwa kwa maroketi na ndege zisizo na rubani za muqawama wa Kiislamu wa Iraq. 

Jana Alkhamisi pia, Mujahidina wa muqawama walishambulia kambi ya kijeshi ya Marekani karibu na eneo lenye visima vya gesi la Koniko mkoani Dayr al-Zawr nchini Syria.

Aidha wanamuqawama hao walishambulia vituo vya kijeshi vya Marekani katika maeneo ya Al-Tanf na Al-Rukban huko nchini Syria.

Tangu kuanza Oparesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa na Marekani kutangaza uungaji mkono wa pande zote kwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina, makundi ya muqawama ya Iraq, Syria na Yemen pia yalitangaza kuwa yatashambulia ngome na maslahi ya Marekani katika nchi hizo za Kiarabu.

Maafisa wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) wamekiri kuwa, kambi za kijeshi za US katika nchi hizo za eneo la Asia Magharibi zimeshambuliwa zaidi ya mara 100 tangu Oktoba 17, na kujeruhiwa makumi ya askari wa nchi hiyo ya kibeberu.

Marekani, muitifaki mkubwa zaidi wa Israel, imekuwa ikiupa silaha na zana kivita utawala wa Kizayuni kwa kiwango kikubwa, tangu Tel Aviv ianzishe hujuma za kinyama dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7.

Tags