WFP yatahadharisha kuhusu mgogoro wa njaa Ukanda wa Gaza
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetahadharisha kuwa Ukanda wa Gaza utakumbwa na mgogoro wa njaa iwapo vita vitaendelea katika eneo hilo.
WFP imetahadharisha kuwa Gaza inakabiliwa na tatizo kubwa la njaa na ripoti zinasema kuwa hali hiyo itakuwa mbaya sana iwapo vita vitaendelea katika eneo hilo. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeongeza kuwa: Gaza itatumbukia katika hatari ya njaa iwapo chakula cha kutosha, maji safi na huduma nyingine za kibinadamu hazitatolewa kwa ajili ya wakazi wa ukanda huo.
Carl Skau Naibu Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) awali alieleza kuwa hali katika Ukanda wa Gaza inazidi kukatisha tamaa.
Ameongeza kuwa: "Wakati wa usitishaji vita wa siku saba huko Gaza tulichunguza hali ya usalama wa chakula katika eneo hilo na kugundua kuwa nusu ya watu wa Gaza walikuwa na njaa."
Skau ameeleza kuwa ukweli mwingine mchungu ni kuwa watu 9 kati ya kila watu 10 huko Gaza, hawali chakula cha kutosha na hawapati chakula kila siku.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa watu zaidi ya 570,000 yaani karibu robo ya wakazi wa Ukanda wa Gaza, wanakabiliwa na njaa kali kutokana na vitisho.