Ugaidi, mbinu ya Israeli ya kukwepa fedheha ya kushindwa kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107048-ugaidi_mbinu_ya_israeli_ya_kukwepa_fedheha_ya_kushindwa_kijeshi
Kushindwa Israel kufikia malengo ya kijeshi katika medani ya vita huko Gaza kumeifanya kugeukia mbinu ya kuwaua kigaidi makamanda wa makundi ya muqawama.
(last modified 2024-01-10T07:41:26+00:00 )
Jan 10, 2024 07:41 UTC
  • Ugaidi, mbinu ya Israeli ya kukwepa fedheha ya kushindwa kijeshi

Kushindwa Israel kufikia malengo ya kijeshi katika medani ya vita huko Gaza kumeifanya kugeukia mbinu ya kuwaua kigaidi makamanda wa makundi ya muqawama.

Katika kipindi cha siku nne za hivi karibuni utawala wa Kizayuni umetekeleza operesheni nne za kigaidi dhidi ya makamanda wa makundi ya muqawama katika eneo. Sayyid Razi Mousavi, mmoja wa makamanda wa Iran nchini Syria, Wissam al-Tawil, mmoja wa makamanda na maafisa mashuhuri wa idara ya operesheni ya Hizbullah ya Lebanon na Saleh al-Arouri, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Hamas, wameuawa shahidi na utawala wa Kizayuni katika siku za hivi karibuni, ambapo Abu Taqawi al-Saeidi, kamanda wa Harakati ya Al-Nujba ya Iraq pia aliuawa shahidi karibuni katika shambulizi la ndege isiyo na rubani ya Marekani nchini humo. Wakati huo huo, katika waraka uliochapishwa na vyanzo vya Kiibrania, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel amevitaka vyombo vya usalama vya utawala huo kuandaa mpango kabambe wa kuwaua kigaidi viongozi wa muqawama.

Mauaji hayo ya kigaidi yamefanyika katika mazingira na kwa madhumuni gani? Mauaji hayo yametekelezwa katika hali ambayo utawala wa Kizayuni katika vita vyake vya miezi 3 dhidi ya Gaza haujaweza kufikia malengo yake makuu mawili ya kijeshi, yaani kuachiliwa huru mateka na kuangamizwa Hamas katika ukanda huo. Kwa upande mwingine, mauaji hayo yamefanywa katika hali ambayo maandamano dhidi ya baraza la mawaziri la Netanyahu yameshtadi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), na wakati huo huo kuanikwa hadharani mivutano na hitilafu zilizopo ndani ya baraza la mawaziri la Netanyahu. Kwa hivyo, ni katika hali kama hiyo, ndipo baraza la mawaziri la Netanyahu likapanga njama za kuwaua makamanda wa mapambano ili kujinusuru na wakati huo huo kupunguza mashinikizo dhidi yao.

Moja ya malengo ya utawala wa Kizayuni katika kutekeleza mauaji hayo ya kigaidi, mbali na manufaa ya  ndani, tunaweza kuashiria mambo mengine mawili: Kufunika ushindi mkubwa wa muqawama na kugeuza mkondo wa mapigano kutoka Hamas na Utawal wa Kizayuni kuelekea Muqawama-utawala wa Kizayuni na Marekani. Kwa hakika, ili kuepusha kushindwa kwake huko Gaza, utawala wa Kizayuni unajaribu kuibua vita vikubwa zaidi katika eneo la Asia Magharibi kwa kuishiriki Marekani moja kwa moja.

Lengo jingine muhimu la utawala wa Kizayuni katika kuwaua makamanda wa muqawama ni kuharibu ari na kudhoofisha miundo ya kamandi ndani ya muqawama, kwa ajili ya kuwarejeshea moyo wa kujiamini askari wa Kizayuni walioshindwa katika medani ya mapambano na askari wa muqawama. Hiyo ina maana kwamba utawala wa Kizayuni unataka kufikia ushindi katika uwanja wa mauaji ya kigaidi na kisaikolojia dhidi ya muqawama ili kufidia kile umeshindwa kukifikia katika uwanja wa mapambano ya kijeshi na wanamuqawama.

 Makamanda wa Muqawama Shahidi Haj Qasim Soleimani (kulia) na Seyyed Razi Mousavi

Nukta ya mwisho ni kwamba, hatua za jeshi la kigaidi la utawala wa Kizayuni katika wiki za hivi karibuni zinaashiria mpango wa Tel Aviv wa kuanzisha kampeni ya kuwaua makamanda wa muqawama katika eneo zima la Asia Magharibi. Lakini ushahidi wa kihistoria unaonyesha kwamba ugaidi hauwezi kudhoofisha mhimili wa muqawama kwa sababu huko nyuma pia makamanda muhimu wa muqawapa waliuawa shahidi na magenge ya ugaidi ya Kizayuni lakini hilo halikuweza kusimamisha mapambano dhidi ya utawala huo wa kigaidi. Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa imethibitisha kwamba ugaidi sio tu haujaweza kuzuia muqawama bali umekuwa na matokeo tofauti na utawala huo ulivyokuwa ukitarajia. Wakati huo huo, utawala huo wa kigaidi unapaswa kukumbuka kwamba subira ya kistratijia ya muqawama si subira isiyo na kikomo na bila shaka ulipizaji kisasi kikali unausubiri utawala huo haramu.