HAMAS: Netanyahu anataka kurefusha vita vya Gaza kwa malengo ya kisiasa
Mwanachama mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kundi hilo la muqawama linataka usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza, lakini Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu anataka vita hivyo viendelee kutokana na sababu zake binafsi na za kisiasa.
Hessam Badran alisema hayo jana Jumapili katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Samaa ya Palestina na kuongeza kuwa, "HAMAS ina hamu ya kusitishwa vita kikamilifu Gaza, lakini Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni anataka kuviendeleza vita hivyo."
Amesema Netanyahu anaendelea kueneza urongo kuhusu vita vya Gaza katika hali ambayo, anajua vyema kuwa ni kitu kisichoyumkinika kuiamaliza na kuitokomeza Harakati ya HAMAS.
Badran amebainisha kuwa: Netanyahu anatanguliza mbele maslahi yake juu ya kila kitu. Ni tishio halisi na la kweli kwa uthabiti wa eneo na dunia, na anataka kurefusha vita ili kufikia malengo binafsi ya kisiasa.
Aidha mwanachama huyo mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS amesema wito wa kuwataka viongozi wa harakati hiyo ya muqawama waondoke katika Ukanda wa Gaza hautilii maanani uhalisia wa mambo; na kwamba utawala huo ghasibu ndio unaotakiwa kuondoka katika ardhi za Palestina unaozikalia kwa mabavu.
Utawala huo pandikizi umeshindwa kufikia malengo yake huko Gaza licha ya kuendelea kuwashambuliwa Wapalestina wa eneo hilo lililo chini ya mzingiro kwa mabomu, makombora na kila aina ya silaha. Malengo yaliyotangazwa ya vita dhidi ya Gaza ni 'kuifuta' Harakati ya HAMAS, kuwakomboa wateka wa kivita wa Israel (wanaoshikiliwa na HAMAS) na kutekeleza mpango wa kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza.
Idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na jeshi katili la Israel huko Gaza tangu Oktoba 7 imepindukia 26,400, na idadi ya waliojeruhiwa ni zaidi ya 64,110.