Feb 03, 2024 07:28 UTC
  • Iraq yatoa onyo baada ya US kufanya mashambulizi ya anga nchini humo

Serikali ya Iraq imelaani vikali mashambulizi ya anga yaliyofanywa na ndege za kivita za Marekani dhidi ya maeneo kadhaa ya nchi hiyo na nchi jirani yake Syria na kusisitiza kuwa, hujuma hizo zimekiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo.

Jenerali Yehya Rasool, Msemaji wa Waziri Mkuu wa Iraq, Mohamed Shia al-Sudani amesema katika taarifa kuwa, "Mashambulizi hayo ya anga yamekanyaga mamlaka ya kujitawala Iraq."

Ameeleza bayana kuwa, hujuma hizo za anga zilizofanywa na jeshi la Marekani jana Ijumaa dhidi ya ngome za makundi ya muqawama nchini Iraq na Syria hazikubaliki, na zimekiuka anga na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.

Rasool aidha amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba Iraq haitageuzwa kuwa sehemu ya kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi yoyote ile hasa nchi jirani.

Afisa huyo mwandamizi wa Jeshi la Iraq amesema Marekani imefanya mashambulizi hayo wakati huu ambapo eneo hili tayari linakabiliwa na hatari ya kupanuka mgogoro uliosababishwa na vita vya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. 

Jenerali Yehya Rasool, Msemaji wa jeshi na Waziri Mkuu wa Iraq, Mohamed Shia al-Sudani

Rasool amesema hatua hizo za Marekani zitakuwa na matokeo hasi kwa usalama na uthabiti wa Iraq na eneo zima la Asia Magharibi kwa ujumla. Kambi na vituo vya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Marekani katika nchi za Syria na Iraq vimeshambuliwa mara zaidi ya 130 na makundi ya muqawama, tangu vilipoanza vita vya Gaza mnamo Oktoba 7 mwaka uliopita.

Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imethibitisha kuwa wanajeshi wake jana Ijumaa walishambulia maeneo 85 katika nchi za Iraq na Syria katika hujuma hizo za anga.

Rais Joe Biden wa Marekani amedai kuwa Washington imechukua hatua hiyo, kama sehemu ya jibu la nchi hiyo kwa shambulio la karibuni la ndege zisizo na rubani kwenye kambi ndogo ya jeshi hilo iliyoko nchini Jordan, lililopelekea askari watatu wa jeshi la Marekani kuangamizwa.

Tags