Feb 03, 2024 12:26 UTC
  • Taarifa ya Jeshi la Syria: Mashambulizi ya Marekani yanalenga kulirejesha kundi la Daesh

Wizara ya Ulinzi ya Syria imesema leo kuwa mashambulizi ya jana ya Marekani katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na Iraq yametekelezwa katika maeneo ambako jeshi la Syria linaendelea kupambana dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.

Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani, CENTCOM imetangaza kuwa jeshi la nchi hiyo mapema leo limeshambulia ngome za makundi ya Muqawama huko Iraq na Syria kujibu mauaji ya wanaeshi 3 wa nchi hiyo katika shambulio la ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi yake ya Mnara wa 22 katika mpaka wa Syria na Jordan.  

Shirika la habari la Farsi limeripoti kuwa, kufuatia mashambulizi hayo Wizara ya Ulinzi ya Syria imetangaza kuwa: "Eneo lililoshambuliwa na Marekani huko mashariki mwa Syria ndiko jeshi la nchi hiyo linakoendesha vita dhidi ya masalia ya kundi la kigaidi la Daesh; na suala hili kwa hakika linatilia mkazo kwamba, Marekani iko bega kwa bega na magaidi na inafanya kila iwezalo kulirejesha kundi hilo kama kibaraka wake katika nchi za Syria na Iraq." 

Mshambulizi ya jeshi la Syria dhidi ya ngome za Daesh nchini humo

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Syria imeongeza kuwa: Hujuma ya vikosi vamizi vya Marekani leo asubuhi haiwezi kuhalalishwa kwa namna yoyote ile, na ni mkakati wenye lengo la kudhoofisha uwezo wa jeshi la Syria na waitifaki wake katika vita dhidi ya ugaidi.  

Mwishoni mwa taarifa yake, Wizara ya Ulinzi ya Syria imesisitiza kuwa: Uvamizi wa Marekani katika baadhi ya maeneo ya Syria hauwezi kuendelea, na jeshi la Syria na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vitaendeleza mapambano dhidi ya ugaidi hadi utakapoangamizwa kikamilifu na kukombolewa  ardhi yote ya Syria kutoka kwenye makucha ya wavamizi na magaidi.  

Takwimu za kamili za idadi ya watu waliouawa katika shambulio hilo la Marekani huko Syria na Iraq bado hazijapatikana, lakini televisheni ya Al Jazeera imevinukuu vyanzo vilivyo karibu na kikosi cha kujitolea cha al Hashd al-Shaabi cha huko Iraq  na kuripoti kuwa watu watatu wameuwa na wengine 11 kujeruhiwa katika shambulio la Marekani dhidi ya makao makuu ya kikosi hicho katika mkoa wa al Anbar.

Mashambulizi ya Marekani mashariki mwa Syria na miji ya Al-Mayadeen na Al-Bukamal pia yamesababisha vifo vya watu 10 na kujeruhi wengine 18.

Tags