Hammond akiri, Uingereza ilihusika kuimarisha Daesh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i10810-hammond_akiri_uingereza_ilihusika_kuimarisha_daesh
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amekiri kwamba nchi yake ilifanya makosa wakati wa vita vya Iraq na kwamba suala hilo limechangia katika kuliimarisha na kulipa nguvu zaidi kundi la kigaidi la Daesh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2016 03:49 UTC
  • Hammond akiri, Uingereza ilihusika kuimarisha Daesh

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amekiri kwamba nchi yake ilifanya makosa wakati wa vita vya Iraq na kwamba suala hilo limechangia katika kuliimarisha na kulipa nguvu zaidi kundi la kigaidi la Daesh.

Philip Hammond amesema katika Kamati ya Masuala ya Kigeni ya Bunge la Uingereza kwamba, kwa sasa maafisa wengi wa chama cha Baadh katika kipindi cha uongozi wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein wanashika nafasi za juu katika kundi la kigaidi la Daesh.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amesema kuwa matatizo mengi ya Iraq ya sasa yanatokana na maamuzi ya maafa ya kulivunja jeshi la Iraq baada ya Marekani na Uingereza kuivamia nchi hiyo mwaka 2003.

Hammond amesisitiza kuwa uamuzi huo ulikuwa makosa makubwa ya kipindi cha baada ya vita.

Matamshi hayo ya Philip Hammond yamekuja baada ya kutolewa ripoti ya kamati ya uchunguzi wa nafasi ya Uingereza katika vita vya Iraq iliyopewa jina la Kamati ya Chilcot iliyoundwa mwaka 2009. Ripoti hiyo imekosoa sana uamuzi wa serikali ya Uingereza kutuma majeshi Iraq na kusema msingi uliotumiwa kuchukua uamuzi huo haukubaliki.