Lebanon kuishtaki Israel katika Baraza la Usalama kwa kuishambulia kwa droni
Serikali ya Lebanon imesema itawasilisha faili la malalamiko dhidi ya Israel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kufuatia hatua ya utawala huo wa Kizayuni kufanya shambulio hatarishi la ndege zisizo na rubani na kuua watu kadhaa kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Najib Mikati, Kaimu Waziri Mkuu wa Lebanon alisema hayo jana Alkhamisi katika taarifa na kueleza kuwa, tayari amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kuwasilisha malalamiko ya Beirut katika Baraza la Usalama kuhusu chokochoko hizo za Israel.
Kwa akali watu saba waliuawa katika shambulizi la droni la Israel siku ya Jumatano dhidi ya jengo la makazi ya watu katika mji wa Nabatieh, kusini mwa Lebanon. Aidha shambulio jingine la Israel lililolenga Adshit kusini mwa Lebanon liliua mtu mmoja na kujeruhi wengine 10.
Mikati amelaani vikali kushtadi uvamizi na uchokozi wa Israel kusini mwa Lebanon, na mauaji mapya ya kimbari yanayofanywa na utawala huo haramu dhidi ya raia wa Lebanon kila uchao.
Huku hayo yakijiri, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani mashambulizi ya hivi karibuni zaidi ya Israel kusini mwa Lebanon yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa wakiwemo watoto wawili, ikiapa kwamba majibu ya harakati ya muqawama yako njiani.
Hizbullah na utawala wa Kizayuni wa Israel zimekuwa zikishambuliana karibu kila siku tangu utawala huo haramu ulipoanza mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya watu wa Gaza mwezi Oktoba mwaka jana.
Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanin inasisitiza kuwa operesheni zake zinalenga kuunga mkono na kuwatetea wapigania ukombozi wa Ukanda wa Gaza.