Jul 11, 2016 07:43 UTC
  • Uchunguzi wa kashfa za ufisadi dhidi ya Netanyahu waanza rasmi

Mwezi mmoja baada ya televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutangaza kuwa, polisi ya utawala huo inaendesha uchunguzi wa siri kuhusiana na kashfa za ufisadi wa fedha dhidi Waziri Mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu, sasa Mwanasheria Mkuu wa utawala huo amesema uchunguzi huo umefunguliwa rasmi.

Ofisi ya Avichai Mandelblit, Mwanasheria Mkuu wa Israel imesema karibuni hivi ripoti ya uchunguzi huo dhidi ya Netanyahu itawekwa wazi, kukiwemo kupokea fedha katika njia zisizoeleweka baada ya kuhifadhi kiti chake katika uchaguzi wa mwaka 2009. Inaarfiriwa kuwa, mbali na madai ya usafishaji wa fedha, moja ya tuhuma kuu zinazomuandama Netanyahu ni kupokea rushwa kutoka kwa bilionea mmoja wa Ufaransa kwa jina la Arno Mimran ambaye mapema wiki hii alipandishwa kizimbani akikabiliwa na kashfa za kufanya udanganyifu katika masuala ya kiuchumi huko Ufaransa. Mahakama hiyo ilimhukumu Mfaransa huyo miaka minane jela au faini ya yuro milioni moja. Mimran alipatikana na hatia ya kufanya uharibifu mkubwa wa kiuchumi wenye thamani ya dola bilioni moja, kati ya mwaka 2008 na 2009 katika moja ya kesi dhidi yake. Bilionea huyo wa Kifaransa amekiri kwamba, baadhi ya fedha hizo zilitumbukizwa katika akaunti ya benki ya Netanyahu, kama njia ya kuzisafisha na kwamba fedha hizo zilitumika kwa masuala binafsi ya Waziri Mkuu huyo wa Israel.

Tags