Askari wa Israel waendelea kuangamizwa na wanamuqawama Gaza
Wanajeshi wengine watano wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameangamizwa katika shambulizi la ulipizaji kisasi lililofanywa na Mujahidina wa Brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS katika Ukanda wa Gaza.
Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wanajeshi hao wa Kizayuni waliuawa jana Ijumaa katika makabaliano ya nchi kavu na wanamuqawama huko kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Taarifa ya Izzuddin al-Qassam imeeleza kuwa, askari wengine 12 wa Israel wamejeruhiwa katika makabiliano hayo makali yaliyojiri karibu na lango la kuingia kwenye barabara za chini ya ardhi, mashariki mwa Rafah.
Haya yanajiri siku chache baada ya wapiganaji wa Qassam kushambulia mkusanyiko wa wanajeshi wa Israel katika kivuko cha Kerem Shalom na viunga vyake, kwa kutumia mfumo wa maroketi ya masafa mafupi wa Rajoom na kuangamiza watatu miongoni mwao.
Aidha hivi karibuni, wanamapambano wa Brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la HAMAS walifanya shambulizi jingine la kuvizia na kuangamiza wanajeshi zaidi ya 10 wa Kizayuni mashariki mwa Khan Yunis, Gaza.
HAMAS inasisitiza kuwa, operesheni za wanamuqawama wa Palestina zimetuma ujumbe wa tahadhari kwa Wazayuni kwamba, chokochoko zozote za utawala huo pandikizi zitajibiwa kwa nguvu na matokeo yake yatakuwa mabaya.