UNRWA: Akiba ya chakula kusini mwa Ghaza inakaribia kwisha kabisa
May 13, 2024 00:34 UTC
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetoa indhari kwamba, ikiwa misaada ya kibinadamu haitaingizwa Ghaza, hakutakuwa na chakula chochote cha kuwagaia wakazi wa eneo hilo lililowekewa mzingiro.
UNRWA) ilisisitiza kupitia taarifa iliyotoa jana Jumapili kuwa iwapo msaada wa chakula haungepelekwa Ukanda wa Ghaza hadi kufikia hapo jana, baa la njaa na kukosekana kwa chakula kutahatarisha maisha ya makumi ya maelfu ya raia wa Palestina.
Kuhusiana na hilo, Georgios Petropoulos, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) katika Ukanda wa Ghaza ametangaza kuwa, kutokana na kuendelea kuwekwa vizuizi kwenye vivuko vya mpakani kutokea Israel kuelekea Rafah, fungu la chakula linaotolewa kwa wakimbizi wa kusini mwa Ghaza limemalizika.
Kabla ya hapo, Francesca Albanesse, ripota maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya Palestina, naye pia alieleza kuwa hakuna sehemu yoyote iliyo salama katika Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kwamba utawala wa Israel unakiuka sheria za kimataifa na unapewa kinga na madola makubwa.
Licha ya upinzani wa kimataifa, siku ya Jumatatu ya tarehe 6 Mei, baraza la mawaziri la vita la utawala wa Kizayuni liliidhinisha uvamizi na shambulio la ardhini dhidi ya mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Ghaza; na siku ya Jumanne, jeshi la utawala huo likaanzisha mashambulio dhidi ya mji huo.
Baada ya kuvamia kivuko cha mpakani cha Rafah siku ya Jumanne iliyopita na kusimamisha uingizaji misaada katika Ukanda wa Ghaza, utawala ghasibu wa Kizayuni unaendelea kufanya mauaji ya kimbari, kuwazingira na kuwatesa kwa njaa Wapalestina wa eneo hilo.
Wakati huohuo, kutokana na kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza, Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa: tangu tarehe 7 Oktoba 2023 hadi sasa, karibu Wapalestina elfu 35 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na utawala huo.../
Tags