Makumi ya Wapalestina wauawa katika hujuma za Israel Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i111758-makumi_ya_wapalestina_wauawa_katika_hujuma_za_israel_gaza
Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zimefanya mashambulizi mapya ya anga dhidi ya maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza na kuua shahidi makumi ya Wapalestina, wakiwemo watoto wadogo na wanawake.
(last modified 2024-05-14T07:35:27+00:00 )
May 14, 2024 07:35 UTC
  • Makumi ya Wapalestina wauawa katika hujuma za Israel Gaza

Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zimefanya mashambulizi mapya ya anga dhidi ya maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza na kuua shahidi makumi ya Wapalestina, wakiwemo watoto wadogo na wanawake.

Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, kwa akali Wapalestina 20 wameuawa shahidi katika hujuma za anga zilizolenga kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, katikati ya Gaza.

Habari zaidi zinasema kuwa, makumi ya Wapalestina wengine wa Gaza wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyoanza tangu usiku wa kuamkia leo.

Kanali ya televisheni ya al-Jazeera imetangaza kuwa, makumi ya Wapalestina wameuawa pia katika mashambulizi mengine ya Wazayuni yaliyolenga kambi ya wakimbizi ya Jabalia, na katika jiji la Beit Lahia, kaskazini mwa Gaza.

Mmoja wa wakazi wa Jabalia amewaambia waandishi wa habari kuwa, "Raia wanakimbia huku na kule barabarani, tumehamishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine, hatujui tena pa kwenda."

Image Caption

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameshadidisha mashambulizi ya umwagaji damu huko Gaza katika hali ambayo, Wapalestina hapo kesho wanaadhimisha Siku ya Nakba.

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, yaani tarehe 14 Mei 1948, walianza kuhamishwa kwa nguvu mamia ya maelfu ya Wapalestina katika ardhi za mababu zao na kuasisiwa utawala bandia wa Israel.