Maelfu ya Wapalestina waandamana katika kumbukumbu ya siku ya Nakba
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i111800-maelfu_ya_wapalestina_waandamana_katika_kumbukumbu_ya_siku_ya_nakba
Maelfu ya wananchi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu wameandamana kwa mnasaba wa Siku ya Nakba ambayo inakumbusha uvamizi, mauaji ya kimbari, ukatili na jinai za Wazayuni katika ardhi za Wapalestina.
(last modified 2024-05-15T10:07:55+00:00 )
May 15, 2024 10:07 UTC
  • Maelfu ya Wapalestina waandamana katika kumbukumbu ya siku ya Nakba

Maelfu ya wananchi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu wameandamana kwa mnasaba wa Siku ya Nakba ambayo inakumbusha uvamizi, mauaji ya kimbari, ukatili na jinai za Wazayuni katika ardhi za Wapalestina.

Tarehe 15 Mei 1948, Wazayuni walianza kuikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina na kuweka jiwe la msingi la machafuko, jinai, ukosekanaji wa amani na ukaliaji ardhi kwa mabavu katika eneo la Asia Magharibi.

Katika historia ya PalestinaJumatano ya leo tarehe 15 Mei inajulikana kuwa ni Siku ya Nakba.

Kwa mnasaba huo, leo shule, vyuo vikuu, maeneo ya umma na biashara katika miji mbalimbali ya Ukanda wa Gaza zilifungwa na wananchi kujitokeza na kushiriki katika maandamano ya siku hiyo ya Nakba.

 

Neno 'Nakba' linakumbusha mambo mawili mabaya mno katika kumbukumbu za Wapalestina na fikra za waliowengi. Mosi, ni kuundwa utawala ghasibu wa Israel mwaka 1948 na pili kufukuzwa zaidi ya Wapalestina laki nane katika ardhi yao ya asili.

Siku ya Nakba si nembo ya maafa tu yaliyotokea katika mwaka huo katika ardhi ya Palestina, bali ni dhihirisho la matatizo na masaibu liliyotwishwa taifa hilo katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Yawm an-Nakba (Siku ya Nakba) ni simulizi ya mauaji ya kizazi ambayo ilifuatiwa na kuharibiwa sehemu kubwa ya misingi ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na haki za Wapalestina ili kuandaa uwanja na kufungua njia ya kutangazwa uwepo wa utawala mmoja bandia na haramu.