Jun 13, 2024 07:38 UTC
  • UN: Watoto 3,000 katika hatari ya kupoteza maisha kwa utapiamlo Gaza

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeonya kuwa, takriban watoto 3,000 wa Kipalestina wapo katika ncha ya kuaga dunia mbele ya jamaa zao kwa kukosa matibabu ya utapiamlo wa kiwango cha juu kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Adele Khodr, Mkurugenzi wa UNICEF katika eneo la Asia Magharibi na Kaskazini mwa Afrika ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa, vituo viwili tu kati ya vitatu vya kuwatibu watoto wenye utapiamlo wa kiwango cha juu Gaza, vikiwa ndivyo vinafanya kazi.

Khodr amesema, watoto hawa 3,000 wasipotibiwa haraka iwezekanavyo, watatumbukia katika hatari ya kuwa wagonjwa zaidi na kupata matatizo makubwa na hatari ya kiafya, na waingie kwenye orodha inayozidi kurefuka wavulana na wasichana waliouawa kwenye janga hili lisilo la kiutu na la kutengenezwa na mwanadamu. 

Wakati huo huo, Shirika la Afya Dunia (WHO) limetahadharisha kuhusu hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa, watoto zaidi ya 8,000 wenye chini ya miaka 5 huko Gaza wanasumbuliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu kutokana na vita vya kikatili na vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala haramu wa Israel.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la UN, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuwa badala ya kuwa na maisha ya utotoni yenye furaha, watoto huko Ukanda wa Gaza wanapitia hofu, majonzi na ukatili.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa,  zaidi ya Wapalestina elfu 37,000, wakiwemo watoto zaidi ya 15,500 wameuawa shahidi tangu Oktoba 7, 2023,  na karibu asilimia 70 ya miundombinu ya kiraia ya Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na shule, nyumba za makazi na hospitali zimeharibiwa vibaya katika maeneo wanapoishi watu Gaza wasio na ulinzi.

Tags