Matokeo ya operesheni 2,500 za kijeshi za Hizbullah ya Lebanon dhidi ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu
Katika siku 300 zilizopita tangu kuanza hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza, Hizbullah ya Lebanon imelenga shabaha maeneo mbalimbali utawala huo katika operesheni za kijeshi 2,500.
Imepita zaidi ya miezi kumi 10 tangu utawala vamizi wa Israel uanzishe vita vya mauaji ya halaiki huko Ukanda wa Gaza mapema Oktoba 7 mwaka jana (2023), dhidi ya wananchi madhulumu wasio na hatia wa Palestina huko Ukanda wa Gaza.
Katika kipindi hicho, utawala wa Kizayuni umefanya jinai kubwa zaidi katika historia ya mwanadamu dhidi ya raia madhulumu wa Gaza. Kuuawa shahidi takriban watu 40,000 na kujeruhi zaidi ya watu 91,000 pamoja na kushambulia vituo vya matibabu na hospitali, shule, maeneo ya ibada na kuwaua kwa njaa raia, haswa watoto, ni sehemu ya uhalifu huo. Marekani na Magharibi pia ni washirika katika jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza kutokana na himaya na uungaji mkono wao kwa utawala huo wa kifedha na kisilaha.
Katika hali ambayo hadi sasa, isipokuwa Yemen, hakuna nchi nyingine iliyochukua hatua za kijeshi dhidi ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi wa Gaza, Hizbullah ya Lebanon imefanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya utawala wa Kizayuni tangu tarehe 7 Oktoba 2023 na inaendelea kutekeleza mashambulizi yake. Mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya ngome na maeneo ya utawala wa Kizayuni yanaendelea kufanywa na Hizbullah.
Hadi sasa Hizbullah ya Lebanon imeshatekeleza operesheni 2,500 za kijeshi dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Lengo kuu la operesheni za kijeshi za Hizbullah ya Lebanon ni kuishughulisha sehemu kubwa ya jeshi la Kizayuni katika eneo la kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kupunguza umakini wa jeshi la utawala huo wa Kizayuni kwa Ukanda wa Gaza. Kwa hakika Hizbullah ya Lebanon iliingia katika vita dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa kujua na kwa kukusudia, na wapiganaji wa Hizbullah ya Lebanon nao wameuawa shahidi kwa ajili ya kuwalinda wananchi madhulumu wa Gaza.
Hizbullah ilitangaza kwamba itaifanya safu yake ya mbele kuwa hai na amilifu hadi kutakapokuwa na usitishaji mapigano huko Gaza na itaendelea na mashambulizi ya kila siku dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Hadi sasa makumi ya wanachama na makamanda wa Hizbullah ya Lebanon wameuawa shahidi kutokana na mashambulizi ya Wazayuni. Fuad Shukr, kamanda mwanadamizi wa Hizbullah ya Lebanon ni mmoja wa makamanda waliouawa shahidi wiki iliyopita kutokana na mashambulizi ya Wazayuni.
Hata hivyo mashambulizi ya kila siku ya Hizbullah ya Lebanon dhidi ya Wazayuni pia yamesababisha hasara kubwa kwa utawala huo. Katika operesheni 2,500 za Hizbullah ya Lebanon dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni, zaidi ya Wazayuni 2,000 wameuawa na kujeruhiwa, na walowezi 230,000 wa Kizayuni katika maeneo ya kaskazini mwa ardhi hiyo inayokaliwa kwa mabavu wameyakimbia makazi yao.
Pia katika kipindi hicho, Hizbullah imetungua ndege nane zisizo na rubani za utawala wa Kizayuni na kulenga makao 391 na kambi 102 za kijeshi. Kadhalika katika kipindi hicho, wapiganaji wa Hizbullah walilenga sehemu ya kutunzia silaha za jeshi la Israel, puto za kijasusi, magari ya kijeshi, vituo vya mipakani, vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kambi za kijeshi.
Justin Crump, mtaalamu wa masuala ya kijeshi mwenye makao yake nchini Uingereza anasema, Hizbullah labda ndiyo mpinzani mkali zaidi wa Israel hivi sasa, na inaweza kusababisha mshangao mkubwa iwapo mzozo huo utaenea.
Moja ya matokeo muhimu ya mashambulizi ya Hizbullah ya Lebanon dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ilikuwa ni kuundwa kwa "umoja wa kambi". "Umoja wa Kambi" ulijumuisha ushirikiano wa Hizbullah, Hamas, Jihadul Islami, Wayemen na makundi ya Iraq katika kuihami na kuitetea Gaza dhidi ya utawala wa Kizayuni. Umoja wa Kambi sambamba na kuleta mshikamano na umoja baina ya makundi ya muqawama, ulizushha wasi wasi mkubwa kwa Wazayuni na pia kuzidisha uungaji mkono wa Wamagharibi hususan Marekani kwa utawala wa Kizayuni ambapo mfano wa wazi ni mashambulizi ya Marekani dhidi ya Wayemeni.