Assad akosoa waungaji mkono wa makundi ya kigaidi
Rais wa Syria amesema kuwa uungaji mkono wa baadhi ya nchi kwa suala la ugaidi ndiyo sababu ya machafuko na kuwepo ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla.
Rais wa Syria ameyasema hayo katika mazungumzo na Alauddin Buroujerdi Mwenyekiti wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran yaani Bunge huko Damascus mji mkuu wa Syria.
Rais Bashar al Assad amesema kuwa ushindi wa jeshi la Syria katika mapambano dhidi ya ugaidi yamewapa heshima wananchi wa Syria katika njia ya mapambano na kuongeza kuwa, uungaji mkono kwa suala la ugaidi unapaswa kukomeshwa.
Rais Bashar al Assad amesema mafanikio ya jeshi la Syria na vikosi waitifaki katika vita dhidi ya magaidi huko Halab kaskazini mwa nchi hiyo, yanatoa taswira ya baadaye ya eneo hili kwa maslahi ya muqawama.
Rais wa Syria amebainisha kuwa mustakbali wa eneo la Mashariki ya Kati utaainishwa na watu wa mataifa ya eneo hili ambao wamesimama kidete kukabiliana na siasa za nchi zinazounga mkono ugaidi ambao pia wamejitolea kupigania na kulinda uhuru wa nchi zao.