Hizbullah Lebanon: Wanamuqawama wetu wanapambana na mabeberu wa dunia Syria
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu nchini Lebanon Hizbullah, amesema kuwa wanamapambano wa harakati hiyo wanapambana na mabeberu wa dunia nchini Syria.
Sheikh Naim Qassim aliyasema hayo Jumatano ya jana ambapo sanjari na kusisitiza juu ya kuendeleza mapambano nchini Syria amesema kuwa, harakati hiyo inapambana na mataifa ya kibeberu ndani ya taifa hilo. Sheikh Naim Qassem ameongeza kuwa, hadi sasa harakati ya Hizbullah kwa kushirikiana na waitifaki wake hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imeweza kukwamisha njama zote za mabeberu wa dunia za kutaka kuiangusha serikali halali ya Syria.
Amesisitiza kwa kusema kama ninavyonukuu: "Kamwe Hizbullah haitoiacha Syria na daima itaendelea kupambana na magaidi vibaraka wanaotumikia malengo machafu ya mabeberu ndani ya nchi hiyo." Mwisho wa kunukuu. Aidha amesisitiza kwa kusema: "Ikiwa zipo baadhi ya pande zinazodhania kwamba Hizbullah tutashindwa, basi zinatakiwa kufahamu kwamba, mapambano yetu na magaidi na pia wavamizi wa taifa la Syria yataendelea siku zote na kamwe hatutachoka." Mwisho wa kunukuu.
Inafaa kuashiria kuwa, wanamapambano wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah wamekuwa wakishiriki operesheni za jeshi la Syria kwa miaka kadhaa sasa dhidi ya magaidi na matakfiri wanaopata himaya ya madola ya Magharibi, Israel, Uturuki, Saudia na Qatar, operesheni ambazo zimetoa pigo kubwa kwa magaidi hao na mabwana zao.