Operesheni ya kuukomboa mji wa Raqqah Syria yaanza
Askari wa chama cha Umoja wa Kidemokrasia cha Wakurdi wa Syria kimeanzisha operesheni ya kuukomboa mji wa Raqqah wa kaskazini mwa Syria kutoka mikononi mwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS).
Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kukinukuu chama hicho kikitangaza jana Jumapili katika mji wa Ain Isa, kaskazini mwa Raqqah kwamba operesheni ya kuukomboa mji huo ambao magai wa Daesh wameufanya kuwa ngome yao kuu nchini Syria imeanza na kinataraji Uturuki itaacha kuingilia mambo ya ndani ya Syria.
Vikosi vya Wakurdi wa Syria vimesisitiza kuwa, wananchi wa nchi hiyo wakazi wa Raqqah wana uhakika kuwa mji wao utakombolewa, na magaidi wote wa Daesh watafurushwa mjini humo.

Taarifa ya chama hicho imeongeza kuwa, mji wa Raqqah una jamii za watu wote, Waarabu, Wakurdi na Waturkeman na wote hao wanashiriki katika operesheni za kuukomboa mji huo.
Vile vile kimeyataka mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya kibinadamu kwa kuwasaidia wananchi wa mji wa Raqqah wanaoteseka mikononi mwa genge la kitakfiri na kigaidi la Daesh.
Operesheni ya chama hicho ya kuikomboa Raqqah iliyopewa jina la "Hasira za Furat" ilianza usiku wa Jumamosi Novemba 5, 2016 na askari karibu 30 elfu wanashiriki kwenye operesheni hiyo.