Daesh, wananyofoa viungo vya mateka na kuvitumia katika miili yao
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i2161-daesh_wananyofoa_viungo_vya_mateka_na_kuvitumia_katika_miili_yao
Wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, wamekuwa wakinyofoa viungo vya mateka wanaowashikilia na kuvitumia kwenye miili yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 29, 2016 09:57 UTC
  • Daesh, wananyofoa viungo vya mateka na kuvitumia katika miili yao

Wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, wamekuwa wakinyofoa viungo vya mateka wanaowashikilia na kuvitumia kwenye miili yao.

Kuongezeka idadi kubwa ya majeruhi wa kundi hilo la kitakfiri nchini Iraq, kumewafanya wanachama wa Daesh kunyofoa viungo vya wafungwa bila ridhaa yao, na kuvitumia wao. Hayo yamethibitishwa na gazeti la El Mundo la nchini Uhispania, ambalo limeongeza kuwa mbali na kunyofoa kwa nguvu viungo vya wafungwa, wanachama wa kundi la Daesh wamekuwa wakiwalazimisha pia wafungwa hao kutoa damu zao, ambazo huzitumia kwa Madaesh waliojeruhiwa. Limeongeza kuwa, wafungwa ambao wamehukumiwa adhabu ya kifo na kundi hilo, huwa wanacheleweshwa kunyongwa ili kustafidi na damu na viungo vyao kwa ajili ya wanachama wake. Gazeti hilo la Kihispania limefafanua zaidi kuwa, kundi la Daesh limegeuka na kuwa muuzaji mkubwa wa viungo vya binaadamu, suala ambalo linatia wasi wasi mkubwa. Inaelezwa kuwa, Daesh imeasisi kituo ambacho kinaongozwa na wataalamu kutoka Ujerumani katika mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa, Iraq ambacho kinajihusisha tu na shughuli za kunyofoa viungo vya binaadamu na kuvisafirisha nje ya nchi. Tangu mwezi Juni mwaka 2014, mji wa Mosul umekuwa ukidhibitiwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, sanjari na magaidi hao kuwalazimisha wakazi wake kurudi mjini hapo kwa lengo la kuimarisha zaidi satwa yao.