Ndege za kivita za Uturuki zauwa raia kaskazini mwa Syria
(last modified Fri, 23 Dec 2016 06:48:29 GMT )
Dec 23, 2016 06:48 UTC
  • Ndege za kivita za Uturuki zauwa raia kaskazini mwa Syria

Makumi ya raia wameuliwa katika mashambulizi ya ndege za kivita za Uturuki kaskazini mwa Syria.

Kundi moja la waangalizi wa haki za binadamu limetangaza kuwa raia 47 waliuawa katika mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za Uturuki hapo jana katika ngome za kundi la kigaidi la Daesh kenye eneo la al Baab huko Syria. Watoto 14 na wanawake 9 ni miongoni mwa raia waliouliwa kwenye hujuma hiyo ya ndege za kivita za Uturuki.

Itakumbukwa kuwa, tarehe 24 mwezi Agosti mwaka huu Ankara ilituma vifaru na wanajeshi kaskazini mwa Syria kutekeleza operesheni yake iliyojulikana kwa jina la "Bamba la Furati" katika juhudi za kile ilichokitaja kuwa ni kuwaangamiza magaidi wa Daesh na wapiganaji wa Kikurdi wa PKK.  

Vifaru vya Uturuki vikiingia katika mji wa mpakani wa Syria wa Jarablus

Viongozi wa Damascus wamelaani mashambulizi ya anga na nchi kavu ya Uturuki huko Syria na kueleza kuwa, serikali ya Ankara inayakandamiza makundi ya Kikurdi hususan Wakurdi walio dhidi yake huko Syria kwa kisingizio cha kupambana na Daesh.

Uturuki inadai kuzishambulia ngome za kundi la Daesh huko Syria huku duru za Syria na Russia zikiwasilisha nyaraka na ushahidi mkubwa kuhusu uungaji mkono mkubwa wa Uturuki kwa kundi hilo la kigaidi.