UN: Ghasia na ugaidi vimeua raia karibu 7000 Iraq, 2016
Umoja wa Mataifa umesema takriban raia elfu 7 wameuawa katika mapigano na mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh/ISIS mwaka uliomalizika wa 2016 nchini Iraq.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq (UNAMI) umesema kuwa, raia 6,878 wameuawa kutokana na mashambulizi na jinai za kutisha za ISIS katika nchi hiyo ya Kiarabu mwaka 2016 pekee. Taarifa ya UNAMI imeongeza kuwa, raia wengine 12,388 wamejeruhiwa katika hujuma na jinai hizo za Daesh mwaka uliomalizika.
Hata hivyo UN imesema takwimu hizo hazijajumuisha idadi ya wahanga wa jinai za Daesh katika mkoa wa Anbar, magharibi mwa nchi, katika miezi ya Mei, Julai, Agosti na Disemba. UNAMI imesema kuwa, raia 386 wameuawa na wengine zaidi ya elfu moja kujeruhiwa katika hujuma za kigaidi katika mkoa wa Ninevah na mji mkuu Baghdad mwezi Disemba 2016 pekee.
Kwa mujibu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq (UNAMI), raia 7,515 waliuawa katika ghasia, mapigano na hujuma za kigaidi nchini Iraq mwaka 2015.
Hii ni katika hali ambayo hadi hivi sasa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani umeshindwa kupata mafanikio yoyote ya maana katika madai yake ya kupambana na Daesh nchini Iraq. Marekani na waitifaki wake katika eneo wanadai kupambana na magaidi wa Daesh licha ya baadhi ya ripoti kuonesha kuwa, Washington na Saudi Arabia zilikubaliana kuwahamisha magaidi wa Daesh kutoka Mosul Iraq na kuwapeleka mashariki mwa Syria.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi alisema vikosi vya jeshi la nchi hiyo vikishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi vitachukua miezi mitatu kuwatimua magaidi wa Daesh katika maeneo yote ya nchi hiyo.