Saudia yaendelea kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel
Kufuatia kuongezeka wasiwasi kuhusu kuimarika ushawishi wa Iran katika eneo baada ya kutiwa saini mapatano ya nyuklia, Israel na Saudia zimezidi kukurubiana ili kukabiliana na hali hiyo.
Tovuti ya Kizayuni ya National News imeandika kwamba ujumbe wa ngazi za juu wa Israel ulitembelea Saudia wiki chache zilizopita. Ripoti hiyo imedokeza kuwa hii haikuwa mara ya kwanza kwa ujumbe wa wakuu wa Israel kutembelea Saudia kwa siri. Moshe Ya'alon Waziri wa Vita wa Utawala wa Kizayuni mwezi uliopita wa Februari akiwa nchini Ujerumani katika Mkutano wa Usalama wa Munich alisema kuwa, Israel iko katika mkakati wa kuwa na uhusiano wa siri na nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi hasa Saudia.
Ushirikiano wa Saudi Arabia na Israel ni jambo ambalo litavuruga usalama wa eneo na mshikamano wa nchi za Kiarabu. Watawala wa Saudia wanajaribu kuhalalisha uhusiano wao na utawala wa Kizayuni.
Siku ya Jumatano, Mohammad bin Nayef Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudia akizungumza katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu huko Tunis, Tunisia alisema nchi za Kiarabu zinakabiliwa na changamoto nyingi za ndani na nje. Alisema tawala za Kiarabu zina jukumu la kukabiliana na changamoto hizo. Pamoja na hayo vitendo vya Saudia ni kinyume cha maneno yake. Saudia inachukua hatua ambazo kivitendo ni dhidi ya mataifa ya Waarabu. Saudia hivi sasa hata haina ile hisia ya utaifa wa Kiarabu. Mfano mzuri wa kupotoka Saudia ni uamuzi wake wa hivi karibuni wa kukata misaada ya kijeshi kwa Jeshi la Lebanon.
Adel al Jubeir Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CNN alidai kuwa Hizbullah ni kundi kubwa la kigaidi duniani na kwamba Iran ndiyo iliyounda Hizbullah.
Wasaudia wanasema msimamo huo ni jibu kwa hatua ya Hizbullah kuondoka katika kile kinachodaiwa kuwa msimamo wa pamoja wa Waarabu na pia kutokana na kuwa sera za Lebanon haziendi sawa na sera za Saudia. Hivi karibuni Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu waliilaumu Lebanon kwa kutounga mkono azimio la jumuiya hiyo dhidi ya Iran.
Ukweli ni kwamba, Saudia haijawahi kuzisaidia nchi za Kiarabu katika wakati wowote mgumu bali Riyadh imekuwa kizingiti kikubwa katika kufikiwa umoja wa serikali za nchi za Kiislamu. Jumuiya ya nchi za Kiarabu iliundwa ili kutetea maslahi ya nchi za Kiarabu lakini sera za Saudia zimepelekea jumuiya hiyo iende kinyume cha maslahi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu. Ikumbukwe kuwa katika vita vya miaka ya 1967 na 1973 vya Waarabu na Israel, Saudia haikutoa himaya yoyote kwa Waarabu.
Watawala wa Saudia wameshindwa hata kubaini maslahi yao hivyo haitazamiwi wataweza kuainisha maslahi ya eneo. Wakuu wa Saudia walimuunga mkono dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein muongo wa 80 wakati alipoanzisha vita vya kulazimishwa dhidi ya Iran. Hii ni katika hali ambayo Saddam alikuwa tishio kwa usalama wa eneo kwani miaka kadhaa baada ya kuivamia Iran aliivamia na kuikaliwa kwa mabavu Kuwait.
Weledi wa mambo wanakiri kuwa Saudia sasa inadhibiti kikamilifu Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na imezibadilisha nchi za Kiarabu kuwa watetezi wa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Baada ya kitendo cha kihalifu cha kuhujumiwa ubalozi wa Saudia mjini Tehran; na pamoja na kuwa wakuu wa Iran walilaani tukio hilo, baraza hilo lilichukua maamuzi dhidi ya Iran. Msimamo kama huo ni dalili ya wazi kuwa baadhi ya nchi za Kiarabu zinatumika kuendeleza sera za Saudia za kuibua mifarakano katika eneo.
Kwa msingi huo kikao cha Jumatano cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kilichukua maamuzi kwa mujibu wa matakwa ya Saudia. Baraza hilo, kufuatia mashinikizo ya Saudia, liliidhinisha sera za Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambayo imeitaja harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hiizbullah kuwa eti ni kundi la kigaidi. Hii ni katika hali ambayo Hizbullah imesimama kidete mara kadhaa na kukabiliana kishujaa na hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel. Ni wazi kuwa Saudia inapuuza tishio na njama za utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu. Sera za Saudia bila shaka ni kinyume na maslahi ya uthabiti na usalama wa eneo la Mashariki ya Kati.