Assad: Marekani kudai inapambana na Daesh huko Syria ni njozi
Rais Bashar al-Assad wa Syria ameutaja muungano wa kijeshi wa Marekani unaodai kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh/ISIS nchini Syria kuwa ni muungano wa kinjozi na wa kuihadaa dunia.
Akiongea na kundi la waandishi wa habari wa Ubelgiji hii leo katika mji wa Damascus, Rais Assad amesema lengo la mungano huo wa Marekani halikuwa kukabiliana na magaidi wa Daesh akisisitiza kuwa, harakati za kundi hilo la kigaidi zilipanuka na kupata nguvu katika kipindi cha operesheni za muungano huo.
Rais Bashar al-Assad wa Syria amefafanua kuwa: "Huo muungano ni wa njozi na uongo, haujakuwa na faida yoyote katika jitihada za kulitokomeza kundi la Daesh nchini. Muungano huo ulishindwa kuwanusuru wananchi wa Syria walipokuwa wanauawa na matakfiri wa ISIS. Aidha naweza kusema kuwa, operesheni za muungano huo sio halali, uwepo wao nchini ni kukanyaga moja kwa moja haki na uhuru wa kujitawala Syria", amesisitiza Rais Assad.
Kadhalika Rais wa Syria ametilia shaka matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Rais wa Marekani Donald Trump kwamba serikali yake itapambana kwa dhati na kundi la kigaidi la Daesh.
Wakati huo huo, kiongozi wa taifa wa Syria amesisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya hautakuwa na nafasi yoyote katika kuijenga tena nchi hiyo ya Kiarabu akisisitiza kuwa, nchi nyingi za Magharibi tangu mwanzo zilitangaza wazi wazi kuyaunga mkono magenge ya kigaidi kama vile al-Nusra na ISIL. "Lazima wabadili sera zao kwanza kwa taifa la Syria", amesema Rais Bashar Assad.
Ni vyema kukumbusha kuwa, mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Assad alisema kuwa, Iran imekuwa muungaji mkono mkuu wa taifa la Syria katika kipindi chote cha mgogoro wa nchi hiyo uliodumu kwa miaka sita sasa.
Hii ni katika hali ambayo, tangu mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu hadi hivi sasa, jeshi la Syria limefanikiwa kukomboa zaidi ya maeneo 30 ya makazi ya raia kutoka kwa genge la wakufurishaji la Daesh.