Jeshi la Syria laangamiza magaidi zaidi ya 2000 wa kitakfiri, Hama
Jeshi la Syria limefanikiwa kuangamiza maelfu ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Jabhat Fateh al-Sham karibu na mji wa Hama, ulio magharibi mwa nchi.
Shirika rasmi la habari la Syria, SANA limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, magaidi 2,200 wa Jabhat Fateh al-Sham wameangamizwa katika operesheni ya chini ya wiki moja iliyofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo ya Kiarabu nje ya mji wa Hama, magharibi mwa nchi, dhidi ya genge hilo la kigaidi ambalo huko nyuma lilijulikana kwa jina la al-Nusra, lenye mfungamano na matakfiri wa al Qaida.
Inaarifiwa kuwa, makamanda waandamizi wa Jabhat Fateh al-Sham ni miongoni mwa magaidi waliouawa katika operesheni hiyo. Habari zaidi zinasema kuwa, jeshi la Syria limefanikiwa kukomboa zaidi ya vijiji 16 vilivyokuwa chini udhibiti wa Daesh katika miji ya Arza, Bazam, al-Samsam na milima ya al-Shaihat, viungani mwa mji wa Hama.
Hii ni licha ya Marekani kushadidisha harakati zake za kijeshi nchini Syria. Washington imetangaza kuwa itapeleka zana zake mpya za kivita nchini Syria sambamba na kutuma askari wengine 1,000 nchini humo, katika hali ambayo kuna wanajeshi zaidi ya 1,000 wa US katika nchi hiyo ya Kiarabu bila idhini ya serikali ya Damascus.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kufuatia mashambulizi makubwa ya makundi ya kigaidi yakiungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kuing'oa madarakani serikali halali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Bashar al Assad, hujuma ambazo hadi sasa zimeshindwa kufikia malengo yake haramu.