Askari 2 wa kulinda amani wa UN wauawa nchini Mali
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i29504-askari_2_wa_kulinda_amani_wa_un_wauawa_nchini_mali
Askari wawili wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali wameuawa katika uvamizi wa genge la kitakfiri lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda kaskazini mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 24, 2017 03:17 UTC
  • Askari 2 wa kulinda amani wa UN wauawa nchini Mali

Askari wawili wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali wameuawa katika uvamizi wa genge la kitakfiri lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda kaskazini mwa nchi.

Duru za kijeshi zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa, askari hao walishambuliwa na wanamgambo hao jana Jumanne walipokuwa wakitembea kwa miguu karibu na mji wa Aguelhok, kaskazini mwa nchi karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.

Mahamat Saleh Annadif, Mkuu wa  Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA) amesema uvamizi huo ni katika wimbi la mashambulizi ya magenge ya kigaidi dhidi ya wanajeshi hao wa kimataifa na kuongeza kuwa, askari hao waliouawa na kujeruhiwa ni raia wa Chad.   

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuitembelea nchi hiyo katika safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipochaguliwa kuwa rais mpya wa Ufaransa tarehe 7 ya mwezi huu wa Mei.

Rais Ufaransa nchini Mali

Katika ziara hiyo Ijumaa iliyopita, Macron alisema kuwa nchi yake itaendelea kubeba mzigo wa kuendesha mapambano ya kijeshi dhidi ya makundi ya wanamgambo wa kitakfiri wenye misimamo ya kufurutu ada kaskazini na magharibi mwa Afrika.

Mapema mwezi huu, askari tisa wa jeshi la Mali waliuawa katika hujuma ya genge la kigaidi lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda katikati ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili , Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa ambacho kilitumwa nchini Mali tangu Julai mwaka 2013, hadi sasa kimepoteza wanajeshi wake zaidi ya 70.