Ripoti: Imarati ilitoa dola bilioni 3 kufadhili mapinduzi ya kijeshi Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i30430-ripoti_imarati_ilitoa_dola_bilioni_3_kufadhili_mapinduzi_ya_kijeshi_uturuki
Gazeti moja la kila siku la Uturuki limeandika kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulitoa kitita cha dola bilioni 3 za Marekani kwa ajili ya kufadhili jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililofeli mwezi Julai mwaka jana 2016 nchini Uturuki.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 13, 2017 23:48 UTC
  • Ripoti: Imarati ilitoa dola bilioni 3 kufadhili mapinduzi ya kijeshi Uturuki

Gazeti moja la kila siku la Uturuki limeandika kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulitoa kitita cha dola bilioni 3 za Marekani kwa ajili ya kufadhili jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililofeli mwezi Julai mwaka jana 2016 nchini Uturuki.

Mehmet Acet, mwandishi wa makala wa gazeti la Yeni Safak la Uturuki amesema Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki alikusudia 'Imarati' alipodokeza huko nyuma kuwa kuna nchi moja ya Kiislamu iliyotumia mabilioni ya dola kujaribu kuangusha serikali ya Uturuki kwa njia isiyo ya kisheria.

Gazeti hilo limeandika kuwa, fedha hizo kutoka Imarati zilitumwa kwenye akaunti za benki za wapambe wa Fethullah Gülen, kiongozi wa kidini na mpinzani wa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan, ambaye anaishi uhamishoni katika jimbo la Pennsylvania, nchini Marekani anayedaiwa kuratibu na kuongoza jaribio hilo la mapinduzi.

Maandamano ya wananchi ya kuunga mkono serikali baada ya kufeli jaribio la mapinduzi Uturuki, Julai 2016

Rais Erdogan amekuwa akisisitiza kuwa, jaribio hilo la mapinduzi lilifanywa na nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, na kwa msingi huo amekuwa akiitaka serikali ya Washington imkabidhi Fethullah Gülen.

Watu wasiopungua 250 waliuawa huku wengine zaidi ya 2,100 wakijeruhiwa katika jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi la Julai mwaka jana. Aidha maelfu ya wafanyakazi wa serikali wakiwemo walimu wamesimamishwa kazi kufuatia tukio hilo.