Syria yakosoa kuendelezwa vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi yake
Bashar Jaafari, Mwakilishi wa Kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amelaani mwendelezo wa vikwazo vya kidhalimu vya nchi za Magharibi dhidi yake na kusema kwamba vikwazo hivyo vimelemaza kabisa shughuli za mashirika ya misaada ya kibinadamu nchini humo.
Vikwazo vya kiuchumi vya upande mmoja vya Marekani na washirika wake wa Ulaya na nchi nyingine kadhaa dhidi ya taifa la Syria vimekuwa na matokeo mengi hasi kwa hali ya kibinadamu na hasa huduma za afya, maji, umeme na masomo ya wanafunzi. Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 baada ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani, Saudi Arabia na washirika wao ikiwemo Uturuki kuanzisha vita vya silaha kwa ajili ya kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar al-Asad wa nchi hiyo. Sambamba na kutekelezwa njama hiyo ya kijeshi na kisiasa ya Marekani dhidi ya Syria, nchi hiyo ya Kiarabu pia inakabiliwa na njama nyingine ya kiuchumi ya nchi za Magharibi kwa lengo la kulilazimisha taifa la Syria lisalimu amri mbele ya matakwa haramu ya madola ya kibeberu ya Magharibi.
Jeremy Hamond, mwandishi wa Marekani na mwanzilishi wa jarida la Foreign Policy Journal anasema hivi kuhusiana na siasa za uhasama na chokochoko za Marekani Mashariki ya Kati: 'Kuendelea siasa za vita na zisizo za kimantiki za viongozi wa Marekani akiwemo Rais Donald Trump wa Marekani nchini Syria ni mchezo hatari ambao bila shaka utakuwa na matokeo hatari kwa Syria, eneo na ulimwengu mzima kwa ujumla.' Mwisho wa kunukuu.
Patrick Wintour mwandishi mwingine wa gazeti la Uingereza la The Guardian na ambaye pia ni mmoja wa wachambuzi mashuhuri wa masuala ya kisiasa kimataifa anasema kuhusu suala hilo kwamba baada ya Wamagharibi kushindwa kijeshi Syria sasa wameamua kuzidisha mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Rais Bashar al-Asad na washirika wake. Kwa hakika vikwazo vya kiuchumi ni mbinu muhimu zaidi inayotumiwa na nchi za Magharibi kwa ajili ya kuzishinikiza nchi zinazokwenda kinyume na matakwa na maslahi yao.
Hiyo ndiyo mbinu ambayo hivi sasa inatekelezwa kwa nguvu zote kwa shabaha ya kuingusha serikali halali ya Rais Bashar al-Asad. Njama za Marekani nchini Syria zinabainisha wazi mipango kabambe iliyowekwa na nchi hiyo kwa ajili ya kuzishinikiza kisiasa na kiuchumi nchi zilizo katika mstari wa mbele wa kukabiliana na siasa za kibeberu za nchi za Magharibi. Syria iko katika mstari wa mbele wa mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na hio ndio maana ikawa inakabiliwa na njama za kila aina kutoka madola hayo ya Magharibi. Uungaji mkono wa kidhahiri na kimaonyesho tu wa Marekani eti kwa demokrasia nchini Syria ni mbinu ya hadaa na ujanja unaotumiwa na nchi hiyo kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Nchi za Magharibi zimezidisha vikwazo vyao dhidi ya Syria katika hali ambayo Marekani, Uigereza na Ufaransa zimekuwa zikiandaa vikao vya kinafiki eti vya marafiki wa nchi hiyo ya Kiarabu. Hii ni katika hali ambayo magaidi na makundi yanayobeba silaha nchini Syria kwa uungaji mkono wa nchi hizohizo za Magharibi yamekuwa yakitekeleza mauaji na jinai za kutisha dhidi ya raia wenzao nchini humo. Kwa ujumla harakati za Marekani na magaidi zinakamilishana kwa ajili ya kuwaua bila ya huruma na kwa umati raia wa Syria. Serikali za Magharibi zimeongeza vikwazo dhidi ya taifa la Syria na kulisababishia msiba mkubwa ambapo kwa sasa imo katika orodha ya nchi zinazokabiliwa na hali mbaya zaidi ya kibinadamu duniani. Hili ndilo jambo lililoashiriwa hivi karibuni na mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa.