Hizbullah: Tutaendelea kuweko Syria hadi hatari ya magaidi itakapoondoka
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33933-hizbullah_tutaendelea_kuweko_syria_hadi_hatari_ya_magaidi_itakapoondoka
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu ambayo iko Syria kwa ombi la serikali ya nchi hiyo, itabakia nchini humo hadi pale hatari ya ugaidi itakapoondoka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 04, 2017 22:05 UTC
  • Hizbullah: Tutaendelea kuweko Syria hadi hatari ya magaidi itakapoondoka

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu ambayo iko Syria kwa ombi la serikali ya nchi hiyo, itabakia nchini humo hadi pale hatari ya ugaidi itakapoondoka.

Mtandao wa al Ahd wa nchini Lebanon jana (Jumatatu) ulimnukuu Sheikh Naim Qassim akisema hayo katika sherehe zilizofanyika kwenye eneo la Sour la kusini mwa Lebanon na kubainisha kuwa: Hizbullah haiwezi kuondoka Syria ila pale itakapokuwa na yakini ya kuangamizwa makundi yote ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani na utawala wa Kizayuni a Israel hata ikibidi kubakia Syria kwa miaka mingi.

Mwanamapambano wa Hizbullah

 

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, utulivu na usalama wa Syria ni sawa na utulivu na usalama wa Lebanon na adui wa nchi zote hizo mbili ni mmoja. Aidha amesisitiza kuwa, Syria lazima ikombolewe na iwe nchi huru ambayo itaendesha mambo yake bila ya kubebeshwa na mtu yeyote.

Sheikh Naim Qassim aidha amegusia namna Israel ilivyokasirishwa na ushindi wa hivi karibuni wa jeshi la Lebanon na vikosi vya muqawama katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani na Israel katika mpaka wa Lebanon na Syria na kuongeza kuwa: Hivi sasa utawala wa Kizayuni hauna tena uwezo wa kubadilisha hali iliyopo katika eneo hili kwa manufaa yake.

Hivi karibuni vikosi vya muqawama na majeshi ya Syria na Lebanon yalifanikiwa kuwafurusha na kuwasafisha kabisa magaidi wa Daesh na Jabhatunnusra katika miinuko ya Arsal ya Lebanon na al Qalamun Magharibi iliyoko katika mpaka wa Syria na Lebanon.