Baada ya marufuku ya miaka 60 hatimaye wanawake Saudia waruhusiwa kuendesha magari
(last modified Wed, 27 Sep 2017 04:49:21 GMT )
Sep 27, 2017 04:49 UTC
  • Baada ya marufuku ya miaka 60 hatimaye wanawake Saudia waruhusiwa kuendesha magari

Baada ya malalamiko ya muda mrefu hatimaye Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia ametoa amri ya kuwapa leseni za kuendesha magari wanawake wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti, amri hiyo itaanza kutekelezwa miezi 10 kuanzia sasa. Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ndio nchi pekee duniani ambayo inawazuia wanawake kuendesha magari. Marufuku hiyo ilianza kutekelezwa tangu mwaka 1967 ambapo mbali na suala hilo, wanawake wa nchi hiyo walinyimwa haki nyingi za msingi na utawala wa kifalme wa nchi hiyo. Aidha kwa mujibu wa sheria za Saudia, mwanamke haruhusiwi kufanya safari peke yake au kufanya shughuli zozote za kifedha. Kadhalika Saudia ilipiga marufuku mwanamke kwenda kwa daktari bila ya idhini ya mume au mmoja wa watu wake wa karibu.

Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia 

Hii ni katika hali ambayo kwa mara kadhaa mashirika ya kutetea haki za binaadamu yamekuwa yakikosoa vikali ukandamizaji huo dhidi ya binaadamu unaofanywa na utawala wa Aal-Saud nchini humo. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, katika kukaribia kumkabidhi madaraka mwanaye, Mohammad Bin Salman hivi sasa Mfalme Salman bin Abdulaziz anakusudia kufuta baadhi ya sheria ambazo zimekuwa zikikosolewa ndani na nje ya nchi, na kwamba lengo kuu la kufanya hivyo ni kumsafishia njia mwanaye huyo asiweze kukabiliana na changamoto zaidi pindi atakapochukua uongozi.

Tags