Katibu Mkuu wa Hizbullah: Vita vijavyo vitaigharimu mno Israel
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema vita vyovyote itakavyoanzisha Israel dhidi ya Lebanon mnamo siku zijazo ni chokochoko ambayo itaugharimu na kuutia hasara kubwa utawala huo haramu wa Kizayuni.
Sayyid Hassan Nasrullah amezungumzia matukio ya eneo hususan vitisho vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na kueleza kuwa Israel haijiingizi kwenye vita vyovyote bila ya kupata ridhaa ya Marekani, lakini kama itafanya upumbavu na kuamua kuanzisha vita, chokochoko zake hizo zitaigharimu na kuihasiri mno.
Katibu Mkuu wa Hizbullah amebainisha kuwa vikosi vya muqawama vinaendelea muda wote kuongeza nguvu na uwezo wake; na hiyo ni haki yao kwa ajili ya kujihami na kuilinda nchi yao.
Sayyid Hassan Nasrullah ameongeza kuwa usiku na mchana Israel imekuwa ikikiuka mipaka ya angani, baharini na nchi kavu ya Lebanon; na hatua za aina hiyo zinamaanisha kuwa utawala huo haramu unajitayarisha kufanya uchokozi dhidi ya Lebanon katika siku za usoni.
Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa vikosi vya muqawama vina uwezo wa kulenga sehemu yoyote ya Israel yakiwemo matanuri nyuklia na vituo vya utafiti wa kibiolojia vya utawala huo ghasibu na kuongeza kuwa hakutokuwepo na mipaka wala mistari yoyote myekundu ya kutovukwa, endapo Israel itaanzisha vita dhidi ya Lebanon.../