Bin Salman: Tutaendeleza hujuma nchini Yemen, tunakusudia kuzuia isitokee Hizbullah nyingine
Mohammad bin Salman bin Abdulaziz Al Saud, Mrithi wa Kiti cha Ufalme nchini Saudia, ameahidi kuendeleza mashambulizi ya mauaji yanayofanywa na nchi yake kuilenga Yemen.
Bin Salman ameyasema hayo leo na kuongeza kuwa, Saudia itaendeleza mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Yemen na kwamba lengo la hujuma hizo ni kuzuia kusiundwe harakati nyingine ya Hizbullah ndani ya taifa hilo. Mrithi huyo wa kiti cha ufalme nchini Saudia na ambaye pia ni rafiki mkubwa wa madola ya Magharibi sambamba na kuonyesha wasi wasi wake juu ya kupanuka na kuwa na nguvu zaidi Harakati ya Kiislamu ya Answarullah katika eneo la Mashariki ya Kati, amedai kuwa hali hiyo inaifanya Yemen iwe hatari zaidi kuliko Lebanon.
Ameongeza kwamba, hivi sasa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon inayoungwa mkono na Iran, ni jeshi kubwa na lenye nguvu nchini Lebanon na Syria. Kadhalika Mohammad bin Salman bin Abdulaziz Al Saud amesisitiza kuwa, Yemen iko katika eneo muhimu la kijografia kama ambavyo pia inasimamia langobahari la Bab-el-Mandeb na kwa msingi huo, kutokea tukio lolote baya katika eneo hilo kuna maana ya kusimamisha asilimia 10 ya biashara ya dunia. Saudia kwa kushirikiana na Marekani, Imarati, Israel na baadhi ya nchi nyengine za Kiarabu na zisizo za Kiarabu, ilianzisha mashambulio makali yaliyoenda sambamba na mzingiro wa kila upande dhidi ya Yemen kuanzia mwezi Machi mwaka 2015.
Hadi sasa zaidi ya watu elfu 12 wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa huku mamilioni ya wengine pia wakilazimika kuyahama makazi yao. Inafaa kuashiria kuwa, Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah imezuia kwa kiasi kikubwa njama za Saudia, Marekani, Israel na waitifaki wao katika eneo, kutokana na kushiriki kwake moja kwa moja katika vita dhidi ya magaidi wa Daesh, Jab'hatu Nusra na mengine kama hayo huko Syria.