UN yashtushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu Imarati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i38775-un_yashtushwa_na_ukiukwaji_wa_haki_za_binadamu_imarati
Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kutokana na kushtadi uvunjwaji wa haki za binadamu katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 10, 2018 12:32 UTC
  • UN yashtushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu Imarati

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kutokana na kushtadi uvunjwaji wa haki za binadamu katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Ripoti ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN imesema vyombo vya dola katika nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi vinatumia mkono wa chuma katika kuwakandamiza wafungwa na wafanyakazi wa kigeni.

Ripoti hiyo yenye kurasa 13 iliyochapishwa Januari 5 inatazamiwa kuwasilishwa katika kikao cha 29 cha Baraza la Haki za Binadamu, kati ya Januari 15 na 26 mwaka huu. Imesema mbali na ukandamizaji, kuna ubaguzi mkubwa dhidi ya wanawake katika nchi hiyo.

Katika ripoti hiyo, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa imeonyesha kusikitishwa na kitendo cha Imarati cha kufeli kuunda taasisi ya taifa ya kutetea haki za binadamu kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.

UN yasema wafanyakazi wahajiri wanakandamizwa Imarati

Imesema mfumo wa sheria nchini humo umefanya kuwa vigumu kwa wafanyakazi wa nchi za nje kuwasilisha malalamiko yao mbele ya vyombo vya sheria.

Mamlaka za UAE zinatuhumiwa na ripoti hiyo kuwatesa watuhumiwa ili kuwalazimisha wakiri kutenda makosa ambayo hawakuyafanya, huku wakinyimwa haki ya msingi ya huduma za afya.

Aidha Umoja wa Mataifa umeonyesha kushtushwa na wimbi la magendo ya watoto wadogo nchini Imarati wanaotumiwa katika biashara haramu ya ukahaba na kisha baadhi yao kufukuzwa nchini pasina taratibu zifaazo kufuatwa.