Syria yaionya Israel isithubutu tena kuingiza ndege zake nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i40375-syria_yaionya_israel_isithubutu_tena_kuingiza_ndege_zake_nchini_humo
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ametoa onyo kali akisema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel usithubutu tena kuishambulia nchi yake vinginevyo itakumbwa na majibu yatakayouweka mdomo wazi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 15, 2018 00:34 UTC
  • Syria yaionya Israel isithubutu tena kuingiza ndege zake nchini humo

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ametoa onyo kali akisema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel usithubutu tena kuishambulia nchi yake vinginevyo itakumbwa na majibu yatakayouweka mdomo wazi.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limemnukuu Ayman Sosan akisema hayo mbele ya waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, wakati wowote utawala wa Kizayuni utakaposhambulia Syria, jeshi la nchi hiyo litatoa majibu makali ambayo yataiweka mdomo wazi Israel.

Mabaki ya ndege ya utawala wa Kizayuni aina ya F16 iliyotunguliwa na jeshi la Syria

 

Tarehe 10 mwezi huu wa Februari 2018, kikosi cha anga cha jeshi la Syria kilimaliza jeuri za angani za utawala wa Kizayuni kwa kutungua ndege ya kisasa ya Israel aina ya F16 na kubadilisha kabisa mlingano wa nguvu za kijeshi katika eneo hili.

Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kabisa kutunguliwa ndege ya kivita ya Israel tangu mwaka 1982 wakati utawala wa Kizayuni ulipoivamia kijeshi Lebanon. Hadi hivi sasa Israel ilikuwa inajigamba kwa nguvu za kijeshi za angani na kujiaminisha kuwa ndege zake za kijeshi haziwezi kutunguliwa.

Baada ya kutunguliwa ndege hiyo ya Wazayuni katika anga ya Syria, chama cha Hizbullah cha Lebanon kupitia Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Sheikh Naim Qassim kilisema kuwa, zile zama za utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya mashambulizi na kuachiwa vivi hivi bila ya majibu zimeisha na kuanzia sasa shambulio lolote la Wazayuni litajibiwa vikali.

Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon

 

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa unafanya mashambulizi ndani ya ardhi ya Syria kila ilipoona magenge ya kigaidi inayoyaunga mkono yameelemewa na mashambulizi huko Syria. Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema, kutunguliwa ndege ya kisasa kabisa ya Israel katika anga ya Syria kumebadilisha kabisa mlingano wa nguvu za kijeshi na kuanzia sasa utawala wa Kizayuni utakuwa unafikiria sana kabla ya kufanya shambulio lolote lile.