Ripoti: Israel imewateka nyara wanawake 15,000 wa Kipalestina
(last modified Wed, 07 Mar 2018 14:15:24 GMT )
Mar 07, 2018 14:15 UTC
  • Ripoti: Israel imewateka nyara wanawake 15,000 wa Kipalestina

Huku dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake hapo kesho, ripoti mpya ya shirika moja la Palestina inaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umewatia mbaroni wanawake wasiopungua 15,000 wa Kipalestina tokea mwaka 1967 hadi sasa.

Ripoti ya Kamisheni ya Wafungwa wa Sasa na wa Kitambo wa Kipalestina imebanisha kuwa, kuna wanawake 65 wa Kipalestina wanaozuiliwa katika magereza ya kuogofya ya Sharon na Damon, chini ya mazingira magumu.

Ripoti ya shirika hilo iliyochapishwa na gazeti la Middle East Monitor imefafanua kuwa, miongoni mwa makumi ya wanawake hao wa Kipalestina wanaouzuiliwa katika jela za kutisha za Israel, 16 ni wasichana wadogo, 11 wagonjwa na 18 ni wanawake walioolewa.

Ripoti hiyo imemnukuu Shireen al-Issawi, dada ya mfungwa mmoja wa kike kwa jina Samer al-Issawi, akisema kuwa dada yake huyo amezuiwa kupokea vitabu akiwa gerezani, ambapo alikuwa akipokea vitabu hivyo kwa shabaha ya kuendelea na kozi aliyokuwa ameianza kabla ya kutiwa nguvuni.

Wanawake wa Kipalestina Ukanda wa Gaza

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za wafungwa la Addameer, Wapalestina 6,500 wanazuiliwa katika jela za Israel tangu Januari mwaka huu hadi sasa, wakiwemo watoto wadogo na wanawake zaidi ya 350.

Wafungwa hao wa Kipalestina wamekuwa wakilalamika kuwa wanateswa na kudhalilishwa katika magereza hayo ya kuogofya ya utawala katili wa Israel.

    

Tags