Netanyahu maji yamfika shingoni; siasa zake zakosolewa hata na Wazayuni
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel anakabiliwa na hali mbaya ya kisiasa kutokana na ukosoaji dhidi ya siasa zake kuongezeka kila siku ambapo sasa maafisa wa zamani wa usalama wa utawala huo ghasibu wamejiunga na safu ya wakosoaji wake.
Maafisa kadhaa wa Israel waliowahi kushika nyadhifa muhimu za kiusalama wamekosoa vikali siasa za Benjamin Netanyahu na kusisitiza kwamba, utawala huo ghasibu kwa sasa unakabiliwa na maradhi hatari kutokana na Nenyahu kuwa Waziri Mkuu wa utawala huo.
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeandika kuwa, Danny Yatom mkuu wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Israel MOSSAD ambaye alishikilia wadhifa huo katika muongo wa tisini na katika duru ya kwanza ya Uwaziri Mkuu wa Netanyahu amemkosoa vikali Netanyahu na kumtaka ajiuzulu wadhifa huo.
Danny Yatom anasema kuwa, Benjamin Netanyahu na manaibu wake wametanguliza mbele zaidi maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya utawala huo.
Zvi Zamir ambaye naye amewahi kuwa Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Israel MOSSAD kuanzia 1968 hadi 1974 amesisitiza kuwa, Israel kwa sasa haiko katika hali nzuri.
Amesema kuwa, yumkini wakati Netanyahu anachukuua hatamu za Waziri Mkuu wa Israel, utawala huo ulikuwa na mapungufu, lakini hivi sasa Waziri Mkuu huyo ameifikisha pabaya mno Israel.
Maafisa hao wa zamani wa usalama wa utawala vamizi wa Israel wanatoa matamshi yao hayo, katika hali ambayo, kwa sasa Benjamnin Netanyahu anakabiliwa na mafaili kadhaa ya ubadhirifu na mara kadhaa amehojiwa na vyombo vya usalama vya Israel.