Oman yasema haiwezi kuvumilia tena chokochoko za UAE
Migogoro inazidi kutokota katika Ghuba ya Uajemi baada ya Oman kuuonya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa haiwezi kuvumilia tena wizi wa turathi zake za kitaifia na haki za uvumbuzi.
Naibu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umma ya Viwanda vya Sanaa za Mkono nchini Oman Isam bin Ali al Rawas amesema: "Majirani wanapaswa kufahamu kuwa subira ya taifa la Oman sasa imefika ukingoni."
Katika mahojiano na Radio ya al-Wisal ya nchi hiyo, afisa huyo ametahadharisha kuwa, Sultan Qaboos wa Oman ana nyaraka ambazo ni kwa madhara ya UAE na anaweza kuzifichua.
Mgogoro baina ya Oman na UAE ulibainikia umma mwaka 2011 wakati Oman iliposambaratisha mtandao wa majasusi wa UAE ambao walikuwa wanalenga kumdhuru Sultan Qaboos. Hivi karibuni Oman ilighadhabishwa na hatua ya UAE ya kuchapisha ramani ambayo ilionyesho kuwa mkoa wa Musandam ni sehemu ya UAE.

Katika tukio la hivi karibuni, televisheni ya UAE ilimuonyesha shakhsia wa kihistoria wa Oman kuwa ni shujaa wa UAE. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Oman imekuwa ikijaribu kujizuia kuingizwa katika mgogoro baina ya Saudi Arabia na waitifakie wake na Qatar. Aidha Oman inapinga uvamizi unaotekelezwa na nchi zinazoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen.
Sera hizo za kujitegemea za Oman zimekuwa zikiikasirisha Saudi Arabia ambayo inataka kuwa mbabe na kiranja wa mataifa yote ya Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi.