Ufaransa yakiri, Syria imeshinda vita vya ndani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47865-ufaransa_yakiri_syria_imeshinda_vita_vya_ndani
Ufaransa na Uingereza ambazo ni nchi mbili wanachama katika Umoja wa Ulaya (EU) tangu mwaka 2011 zikiwa katika muungano wa nchi za Magharibi na za Kiarabu wa kutaka kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria, zimekuwa zikitoa misaada ya pande zote kwa makundi ya waasi na ya kigaidi kwa shabaha eti ya kuipindua serikali ya Rais Bashar Assad.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2018 03:09 UTC
  • Ufaransa yakiri, Syria imeshinda vita vya ndani

Ufaransa na Uingereza ambazo ni nchi mbili wanachama katika Umoja wa Ulaya (EU) tangu mwaka 2011 zikiwa katika muungano wa nchi za Magharibi na za Kiarabu wa kutaka kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria, zimekuwa zikitoa misaada ya pande zote kwa makundi ya waasi na ya kigaidi kwa shabaha eti ya kuipindua serikali ya Rais Bashar Assad.

Lengo kuu la muungano huo lilikuwa kutoa pigo kwa nguzo kuu ya kambi ya mapambano dhidi ya Wazayuni katika eneo la Mashariki ya Kati yaani Syria na kuvunjavunja mnyororo wa kambi hiyo ya muqawama baada ya kusambaratisha nguzo yake kuu. Hata hivyo muungano huo umeambulia patupu katika vita hivyo vilivyosababisha uharibifu mkubwa. Kwani kwa sasa serikali ya Syria na waitifaki wake mbali na kudhibiti hali ya mambo, wanajiandaa kuyafyagia kikamilifu makundi ya kigaidi katika mkoa wa Idlib ambao bado uko mikononi mwa wapiganaji wa makundi ya kigaidi yanaoungwa mkono na kusaidiwa na nchi za Kimagharibi na Kiarabu. Wamagharibi wenyewe sasa wanakiri kwamba, vibaraka wao wanakaribia kuangamizwa kikamilifu. Katika mkondoa huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian  amekiri kwamba utawala wa Syria unashinda vita dhidi ya ugaidi lakini amedai tena kwamba, iwapo kutatumiwa silaha za kemikali nchini Syria, nchi za Magharibi zitaishambulia tena nchi hiyo. Le Drian amedai kwamba: "Hata kama serikali ya Syria itafanikiwa kukomboa Idlib kutoka kwa makundi yanayobeba silaha, lakini mgogoro wa nchi hiyo hautamalizika, na mapigano hayo yanapaswa kukomeshwa kwa njia ya mazungumzo." 

Jean-Yves Le Drian

Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa kuhusu ushindi wa Bashar Assad na serikali ya Syria katika vita vya ndani ya nchi hiyo ni ishara ya kukata tamaa na kukosa matumaini nchini za Magharibi kuhusu mafanikio ya makundi ya kigaidi zinayoyaunga mkono huko Syria. Pamoja na hayo ushahidi unaonesha kuwa, Marekani na washirika wake wa Ulaya wanafanya mikakati ya kuendeleza uingiliaji wao katika masuala ya ndani ya Syria kwa kutumia njia zote zinazowezekana. Kwa sasa nchi hizo zinatumia kisingizio cha uwezekano wa kutumiwa silaha za kemikali katika vita vya kukomboa mkoa wa Idlib kutoka kwa makundi ya kigaidi. Hata hivyo serikali ya Damascus na muitifaki wake mkuu yaani Russia, zimekuwa zikisisitiza kuwa, nchi za Magharibi zinapanga njama ya kutoa madai bandia kwamba jeshi la Syria limetumia silaha za kemikali na kupata kisingizio cha kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia, Sergey Lavrov anasema: "Wachambuzi wengi wa mambo wanaamini kuwa, Marekani ina maslahi katika kudumisha machafuko katika eneo la Mashariki ya Kati ili iweze kuvua samaki katika maji machafu."

Sergey Lavrov

Katika mkondo huo huo Wizara ya Ulinzi ya Russia wiki iliyopita ilitangaza kuwa, inazo taarifa za kiintelijensia zinazothibitisha kuwa, kundi la kigaidi lenye uhusiano na al Qaida linataka kuziingiza nchi za Magharibi katika mapigano ya Idlib huko Syria kwa kutumia silaha za kemikali na kuisingizia serikali ya Damascus.  

Sambamba na hayo manowari za kivita za Marekani zilizosheheni makombora ya Cruise zimepelekwa mashariki mwa Bahari ya Mediterania. Kutokana na harakati hizo Moscow inaamini kuwa, nchi za Magharibi zinataka tena kuishambulia Syria kwa kisingizio cha kutumiwa silaha za kemikali nchini humo. Kwa sababu hiyo tangu Jumamosi iliyopita Russia imechukua hatua inayoonekana kuwa ni tahadhari kwa nchi za Magharibi ya kufanya mazoezi yake makubwa zaidi ya kijeshi ya baharini baada ya kipindi cha Vita Baridi huko mashariki mwa Bahari ya Mediterania na kandokando ya pwani ya Syria.

Manowari ya jeshi la Marekani. 

Kwa msingi huo ni kwamba, licha ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa kukiri kwamba, Syria imeshinda vita vya ndani ya nchi hiyo lakini nchi za Magharibi zinafanya uafiriti wa kutaka kujidhihirisha kwamba bado zina taathira kubwa katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.